Kafyu yapunguzia Waislamu ada na shughuli zilizozoeleka Ramadhan
Na MISHI GONGO
NI Ramadhan ya kwanza kushuhudiwa ambapo waumini wa dini ya Kiislamu hawateweza kutekeleza ada za mwezi huo kama inavyotakiwa na jinsi ilivyozoeleka tangu jadi.
Hali hiyo inatokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na marufuku yaliyowekwa na serikali ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.
Baadhi ya hatua zilizochukuliwa ni kufungwa kwa misikiti, kutotaka nje baada ya saa moja usiku hadi saa kumi na moja alfajiri na zuio linalowataka watu kutojumuika katika makundi.
Miongoni mwa ada za Ramadhan ni waumini kutekeleza swala za usiku msikitini, kujumuika misikitini kwa chakula baada ya kufungua na kuwaalika jamaa na marafiki nyumbani kujumumiaka nao kwa chakula.
Mkazi wa VOK mjini Mombasa Bw Ali Omar amesema Jumamosi anasikitika kuwa hataweza kujumuika na waumini wenzake katika Ramadhani hii.
“Tunasikitika kuwa hatutaweza kutekeleza baadhi ya shughuli kufuatia kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19, lakini nina imani kuwa hali hii ni ya muda,” amesema.
Muumini mwingine Mosab Abdalla, amesema baada ya kufuturu jioni baada ya saumu ya mchana kutwa yeye hupendelea kutembea ili kusaidia katika kusagika kwa chakula.
“Tukimaliza kula hatuwezi tembeza miguu; madaktari hushauri watu kutolala baada ya kula ili kuepuka maradhi,” amesema.
Wengine walioathirika na hali hiyo ni wauzaji vyakula eneo la Marikiti.
Bw Jumaan Hussein amesema wao huuza vyakula kwa waumini jioni.
“Vyakula vyetu tangu jadi tumezoea kwamba tunauza kuanzia saa kumi hadi saa nne usiku, lakini kufuatia kafyu ya kutoroka nje biashara zimelemaa kwa sababu wanunuzi ni wachache mno,” amesema.
Wafanyabiashara hao wa vyakula kama viazi, sambusa, mikate ya sinia, tende, kahawa na kaimati, wamesema hali hiyo imeathiri hali yao ya kiuchumi.