Kagwe aonya wanasiasa dhidi ya siasa za bei ya majani chai
WAZIRI wa Kilimo, Mutahi Kagwe, amewatahadharisha viongozi wa kisiasa dhidi ya kubadilisha mjadala wa bei ya chai kuwa suala la kisiasa na ukanda, akisema changamoto zinazokumba sekta hiyo ni za kiufundi na zinahitaji kushughulikiwa kupitia sera, takwimu, na ubora wa bidhaa na si maneno ya kisiasa.
Akizungumza Novemba 6, 2025 katika eneo la Kanja, Kaunti ya Embu, wakati wa uzinduzi wa vifaa baridi 13 vya kuhifadhi maziwa kwa vyama vya ushirika vya maziwa, Bw Kagwe alisema wanunuzi wa chai hawalazimishwi kununua kutoka eneo fulani, bali huchagua chai kulingana na ubora na ladha wanazotaka.
“Wanunuzi hawalazimishwi kununua chai kutoka eneo lolote. Huchagua wanachokipenda. Wao ndio wanaoamua aina na ubora wa chai wanayohitaji,” alisema Kagwe.
“Masuala ya ladha ya chai si ya kisiasa; ni ya kiufundi,” aliongeza.
Bw Kagwe alisisitiza kuwa soko la chai nchini lipo wazi chini ya Mamlaka ya Wakulima wa Chai Kenya (KTDA), na kwamba hakuna mkulima anayezuiwa kuuza kwa njia fulani pekee.
“Ukihisi bei unayopata si ya haki, tafuta njia ya mauzo ya moja kwa moja. Wewe uko huru kuchagua unakouza. Kazi yangu ni kuhakikisha ubora wa chai unaimarika kote nchini, na ninashirikiana na maeneo ya mashariki kuhakikisha wanapata bei bora,” alisema.
“Tusifanye siasa kuhusu bei ya chai,” aliongeza.
Waziri huyo aliwataka viongozi waache kugawanya wakulima kwa misingi ya kikanda, akionya kuwa maelezo kama hayo yanaweza kuvuruga sekta ya chai, ambayo kihistoria imekuwa nguzo kuu ya uchumi wa Kenya.
“Hatutaki kugawanya sekta hii. Wanasiasa tafadhali, msiwatenge watu kwa misingi ya kanda. Hakuna mgawanyiko. Wajibu wetu ni kuzalisha chai bora na kusaidia maeneo yanayohitaji msaada kufikia viwango hivyo,” alisema Bw Kagwe.
Aidha, Waziri huyo alisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kutoa kauli za kuunganisha na kuwawezesha wakulima na si kuleta mgawanyiko.
Aliongeza kuwa changamoto zinazokumba sekta ya kilimo zinajulikana vyema na wadau wake, hivyo zinapaswa kushughulikiwa kwa njia za kiufundi, si kwa mashindano ya kisiasa.
“Masuala haya ya kilimo hayahitaji siasa. Tunapaswa kuyashughulikia kwa njia za kitaalamu,” alisema.
Bw Kagwe alisisitiza tena kwamba wizara yake imejitolea kulinda sekta zote ndogo za kilimo na akawahimiza viongozi kujielimisha kuhusu masuala ya kiufundi kabla ya kutoa kauli hadharani