Kampuni ya Kikuyu sasa yatengeneza dawa za kupunguza makali ya HIV
NA DANIEL OGETTA
KIWANDA kimoja mjini Kikuyu kimefanikiwa kutengeneza dawa za kupunguza makali ya ukimwi (ARVs) kwa kuzingatia mwongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO), na juma hili kiimetengeneza vidonge milioni tatu.
Mkurugenzi mkuu wa kiwanda hicho kwa jina Universal Corporation, Perviz Dhanani alisema kwamba tayari walipokea vyeti kutoka kwa WHO kuwaruhusu kutengeneza vidonge hivyo kuanzia Novemba 2018.
“Tuna uwezo wa kutengeneza vidonge milioni moja kila siku. Kupewa hati na Shirika la Afya Duniani kunamaanisha twawezapata kandarasi za kimataifa.”
Kiwanda cha Universal ni cha kwanza kupata idhini ya kutengeneza vidonge vya kupunguza makali ya Ukimwi Kenya.
Asilimia 51 ya hisa za kiwanda hicho zilinunuliwa na kampuni ya Bangalore ambayo inamilikiwa na Pharma Strides Shasun mnamo mwaka wa 2016.
Kiwanda cha Universal hutengeneza aina 100 za dawa ambazo huuzwa Kenya, Zambia, Zimbabwe, Malawi, Namibia, Ivory Coast na Sierra Leone.
Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Dawa na Sumu nchini (PPB) Bw Fred Siyoi alisema viwango vya kuzaliswa kwa dawa hizi humu nchini vimeboreshwa kutokana na kuzingatiwa kwa viwango vya uzalishajiwa na kufuatiliwa na mamlaka ya PPB.
“Nafasi za ajira zimeongezeka. Uwezo wa viwanda kuzalisha dawa pia umeimarika,” alisema.
Kundi la kwanza la dawa hizi za kupunguza makali ya HIV lina mchanganyiko wa chembechembe za Nevirapine, Lamivudine na Zidovudine. Kundi hili limeagizwa na Cote d’Ivoire.
Kenya inatumia takriban Sh38 bilioni kila mwaka kuthibiti Ukimwi. Kila mgonjwa anatumia takribani Sh1,800 kila mwezi.
Dhanani alisema kwamba viwanda vya humu nchini vina ugumu wa kupata uagizo wa dawa za kupunguza makali ya HIV kwa kuwa Global Fund na US Presidential Emergency Fund for Aids ndio wafadhili wakuu wa kuagiza dawa kutoka India.
Hata hivyo, akaeleza kwamba Universal haijafanikiwa kupata vibali kutengeneza dawa za kununuliwa na GF wala Pepfar.
Tangazo hili alilifanya Jumatatu iliyopita waziri wa afya Bi Sicily Kariuki alipotembelea kiwanda hicho mjini Kikuyu.
Aliandamana na Katibu mkuu wa utawala Dr. Rashid Aman, mkuu wa PPB Bw Siyoi na Mkurugenzi mkuu wa KEMSA Bw Jonah Manjari na wengine.
Humu Africa, taifa chache sana zinatengeneza dawa za kupunguza makali ya HIV kutokana na dawa za bei nafuu ghali kutoka India.
Uzalishaji wa dawa hizi humu Afrika kwa Waafrika zitaboresha kasi ya WHO kuhakikisha dawa zimewafikia wagonjwa.