Kampuni za kigeni zinazoendesha biashara dijitali kutozwa ushuru zaidi
WIZARA ya Fedha imewasilisha pendekezo jipya linalolenga kutekeleza mageuzi katika utozaji ushuru wa huduma za kidijitali nchini kupitia kuanzishwa kwa ushuru mpya.
Ushuru huo mpya wa asilimia sita (6) utatozwa kampuni za kigeni zinazoendesha biashara nchini kupitia majukwaa ya kidijitali.
Ushuru huo unaojulikana kimombo kama “Significant Economic Presence Tax” (SEPT) utatozwa kwa mitandao ya kutoa huduma za uchukuzi (ride-hailing platforms), kampuni za kutoa uwasilishaji wa vyakula kupitia mfumo wa kidijitali na kazi za kujitolea zinazoendeshwa kidijitali.
Wizara ya Fedha inasema kuwa ushuru huu unalenga kupanua mawanda ya utozaji ushuru kwa lengo la kuongeza mapato ya serikali.
Ushuru huo utachukua nafasi ya Ushuru wa Huduma za Kidijitali (Digitali Service Tax) wa kima cha asilimia 1.5.
“Ushuru huu utalipwa na raia wa kigeni ambao wanachuma mapato nchini Kenya kutokana na utoaji wa biashara zinazoendeshwa kupitia majukuwa ya kidijitali,” inasema notisi kutoka kwa Waziri wa Fedha John Mbadi iliyotumwa kwa vyombo vya habari Jumamosi, Novemba 2, 2024.
Waziri alisema ushuru wa SEPT unalenga kuhakikisha kuwa kampuni za kigeni zinazochuma mapato kwa kutoa huduma za kidijitali nchini zinatozwa ushuru kwa viwango sawa, vinavyolandana na viwango vya kimataifa.
Tangu alipoteuliwa kuongoza wizara ya fedha mnamo Julai mwaka huu, Bw Mbadi ambaye ni mtaalamu wa uhasibu amekuwa akikariri kujitolea kwake kuhakikisha anaongeza viwango vya ukusanyaji mapato kupitia kupanuliwa kwa mawanda ya ushuru badala ya kuongezwa viwango vya ushuru na hivyo kuwaumiza Wakenya.