Kang'ata amkosoa Maraga kuhusu umri wa kushiriki ngono
NA NDUNGU GACHANE
SENETA wa Murang’a Irungu Kanga’ta Jumapili amekejeli matamshi ya Jaji Mkuu David Maraga kwamba magereza yamejazwa matineja wanaotuhumiwa kushiriki ngono wakati wanapovunja ungo ilhali wazee wanaotekeleza dhuluma za kimapenzi wanaendelea kuwa huru.
“Kuna ukiukaji mkubwa wa haki kwa kujaza magereza na matineja ambao hushiriki ngono na matineja wenzao kutokana na ashiki kubwa ya mahaba hasa wanapovunja ungo na kuingia utu uzima,” alisema Bw Maraga wakati wa kuzindua warsha ya siku mbili kuhusu upatikanaji wa haki kwa wanaodhulumiwa kijinsia.
Bw Kang’ata alidai matamshi hayo ni njama ya kufaulisha mjadala wa kupunguzwa kwa umri wa ujana kutoka miaka 18 hadi 16, hali ambayo itawapa wazee nafasi ya kuendeleza dhuluma dhidi ya watoto walio kati ya miaka 17 na 18.
Seneta huyo alisikitika kwamba matamshi ya Bw Maraga kuhusu jinsi mswada wa kupunguza umri wa ujana ulivyokataliwa na bunge ni kudhalilisha asasi hiyo akisema kazi ya mahakama si kuunda sheria bali kuifafanua kortini.
Akizungumza na Taifa Leo Jumapili, Bw Kang’ata alisema matamshi ya Bw Maraga yanaenda kinyume na dini ya Kikristo na anapanga kuwaongoza Wakristo na Waislamu kuandamana dhidi ya afisi yake hadi ajiuzulu.
Vile vile alisisitiza atairai kanisa la Seventh Day Adventist (SDA) kumnyima Jaji Mkuu sakramenti kutokana na matamshi yake mengi yanayokinzana na msimamo wa dini.
“Bw Maraga hafai kudai kuwa anatunga sheria, kazi ambayo inatekelezwa na wabunge ilhali yeye ni jaji. Nitatumia kila mbinu kuhakikisha anajiuzulu kwasababu mapendekezo anayoyatoa kuhusu dhuluma za kimapenzi inazorotesha maadili katika familia. Inasikitisha anaunga mkono kupunguzwa kwa umri wa ngono ilhali inafaa kuongezwa hadi miaka 22,” akasema Bw Kang’ata.