Habari

Kanisa laomba Rais apige breki BBI

December 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

VIONGOZI wa makanisa sasa wanamtaka Rais Uhuru Kenyatta asimamishe mchakato wa kurekebisha katiba, ili kupokea mapendekezo zaidi.

Makundi mbalimbali yamekuwa yakitaka mpango wa kurekebisha katiba usiharakishwe, lakini kufikia sasa, wito wao umegonga mwamba wakisisitiziwa kuwa “meli ilishang’oa nanga”.

Kiongozi anayeondoka wa kanisa la Christ Is The Answer Ministries (CITAM), Askofu David Oginde, Jumamosi alimwambia rais kuwa, kanisa pia lilibaki nyuma wakati safari ya kurekebisha katiba ilipong’oa nanga kwa kasi.

Alikuwa akizungumza katika ibada iliyohudhuriwa na rais ya kumtawaza Askofu Calisto Odede kuwa kiongozi mpya wa CITAM, katika kanisa lililo Karen, Nairobi.

“Nataka kutoa ombi maalumu kwa niaba ya kanisa. Kuna treni ambayo wewe ndiwe dereva. Tangu treni ilipoondoka niliona kanisa limebaki nyuma. Mimi nimeabiri teksi kuwafuata lakini nimeona mambo mengi yamefanyika kwa siku nne. Tafadhali turuhusu tuingie katika treni hii ambayo inaenda kwa kasi mno,” akasema Dkt Oginde.

Hata hivyo, Rais aliposimama kuhutubu hakugusia suala hilo na badala yake akatoa wito kanisa liendelee kushirikiana na serikali kutimiza malengo ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.

“Sote tuko hapa kutumikia, na tunahitaji kushirikiana. Kwa kufanya hivyo tunaweza kuafikia malengo yetu haraka zaidi na kutumiza mahitaji ya wananchi,” akasema Rais.

Makundi mbalimbali na viongozi wamekuwa wakikosoa mchakato wa kurekebisha katiba chini ya Mpango wa Maridhiano (BBI) kwa sababu tofauti.

Kando na suala kuwa baadhi ya maoni yao waliyowasilisha kwa jopo la BBI hayakujumuishwa, kuna wasiwasi kwamba shughuli nzima inaharakishwa wakati ambapo taifa linakumbwa na changamoto tele zinazohitaji kupewa kipaumbele.

Licha ya hayo, watetezi wa mswada wa kurekebisha katiba wakiongozwa na Kinara wa ODM Raila Odinga wanasisitiza muda umeyoyoma kwani wanataka kura ya maamuzi ifanywe mwaka ujao kabla Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Wasimamizi wa mchakato wa kurekebisha katiba walikuwa wamekusanya sahihi takriban milioni tano kufikia mwishoni mwa wiki.

Shughuli hiyo ilikamilika kwa wiki moja pekee, chini ya uangalizi wa maafisa wa utawala wa serikali.

Sahihi hizo zinatarajiwa kuwasilishwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wiki hii, viongozi wakitaka shughuli ya kuzithibitisha iharakishwe ili mswada ujadiliwe na kupitishwa bungeni.

Jumamosi, Naibu Rais William Ruto aliendelea kusisitiza hakuna haraka kurekebisha katiba.

Kulingana naye, kuna masuala yanayohitaji kupigwa msasa katika mswada wa kura ya maamuzi na haifai kuharakishwa.

“Msituharakishe sana. Hii haraka ni ya kuenda wapi? Wakati ule (2010) mlituambia marekebisho ya katiba kama sio sasa ni sasa hivi… Wakati huu mnatuambia meli imeng’oa nanga. Sisi sote tunatafuta jinsi tunavyoweza kutembea pamoja na kutafuta uongozi kwa misingi ya sera za kuimarisha maisha ya Wakenya,” akasema.

Alikuwa akizungumza katika mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Matungu, James Murunga katika Kaunti ya Kakamega.

Kiongozi wa Chama cha ANC, Bw Musalia Mudavadi, ambaye anaunga mkono kura ya maamuzi alimsihi Dkt Ruto abadili nia.

Alitaja suala la BBI kama jipu lililoiva, ambalo sasa linafaa kutobolewa.

“Namwomba Naibu Rais, hili jipu ni chungu. Tusingoje muda mrefu hadi 2022 kwa sababu tutapata majipu mengine. Tufinye hii ya BBI itokomee,” akasema.

Kulingana naye, suala la kurekebisha katiba halifai kuunganishwa na Uchaguzi Mkuu kwa sababu 2022 wanasiasa wanafaa wawe wananadi sera zao kwa wapigakura wala sio kupigia debe mswada wa kurekebisha katiba.

“Hivi sasa hata waekezaji wana wasiwasi kwa vile hawajui hatima ya BBI. Tumalizane na suala hilo mara moja. Acheni Wakenya wapige kura ya ndio au la, hata mimi nimechoka kuzungumza mambo ya BBI,” akasema.

Chama cha ANC awali kilikuwa kinapinga marekebisho ya katiba, lakini Bw Mudavadi alishauriana na Rais Kenyatta kisha baadhi ya mapendekezo ya chama hicho yakajumuishwa kwenye mswada.