Karantini zageuzwa rumande
PETER NGARE Na STEVE NJUGUNA
VITUO vya karantini ambavyo vilifunguliwa kuwatenga walioambukizwa virusi vya corona na waliotangamana nao, sasa vimegeuzwa seli za kuwaadhibu wanaovunja sheria za kukabili janga hilo.
Mnamo Jumatatu, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alikiri kugeuzwa kwa vituo hivyo kuwa vya kuwazuilia wanaovunja sheria za kukabili kusambaa kwa virusi vya corona nchini.
Kauli hiyo ilitiliwa mkazo na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Jumatano alipokuwa akihojiwa redioni.
“Kile tumesema ni kuwa hakuna haja ya kuwapeleka wale wanaovunja kanuni tulizoweka katika vituo vya polisi. Wacha wapelekwe karantini ya lazima,” akasema Rais Kenyatta.
“Tatizo ni kuwa watu wanajitafutia aina hii ya adhabu. Mtu anapokiuka kanuni inachukuliwa kuwa amejiweka kwenye hatari ya kuambukizwa, na hivyo sharti atengwe ili kuwakinga wengine” alisema Msemaji wa Serikali Cyrus Oguna.
Msimamo huu wa Rais Kenyatta, Bw Kagwena Bw Oguna unakiuka sheria ambayo inaeleza adhabu za kisheria zinazopasa kuchukuliwa dhidi ya wanaokiuka kanuni ikiwemo faini au kifungo gerezani.
Wahudumu wa afya wameshutumu hatua hiyo ya kugeuza vituo vya karantini kuwa rumande wakisema huko ni kuvuruga juhudi za kukabiliana na corona.
“Komeni kutumia vituo vya karantini kama rumande za kuwazuia watu bila kuwafungulia mashtaka. Hii ni kuvuruga juhudi za kukabiliana na Covid-19,” akasema Dkt Lukoye Atwoli wa Chuo Kikuu cha Moi.
“Wanaovunja sheria zilizowekwa wanapasa kuchukuliwa hatua za kisheria wala sio kutumia mfumo wa afya kuwaadhibu,” akaeleza Dkt Lukoye kwenye Twitter.
Kulingana naye, kugeuzwa kwa vituo hivyo kuwa mahala pa kuwafungia washukiwa kunawaweka katika hatari ya kuambukizwa virusi hivyo kutokana na misongamano na kukosa kuzingatiwa kwa kanuni za kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo.
Dkt Lukoye alisema pia hatua hiyo inatatiza vita dhidi ya corona kwa kuwaweka watu uwoga badala ya kuwapa ujasiri wa kushirikiana na serikali.
Mazingira ya baadhi ya vituo vya karantini pia ni hatari katika kuchangia maambukizi ya virusi hivyo kutokana na misongamano.
Picha ambazo zimepigwa na waliowekwa vituo hivyo zimeonyesha baadhi wakiwa wamelala sakafuni pamoja na kuwepo kwa misongamano ya watu.
Katibu Mkuu wa Chama cha Watabibu (KCOU) George Gibore, alisema kuwaweka watu karantini kwa lazima kunafanya wanaougua ugonjwa wa Covid-19 waonekane kama wahalifu.
“Serikali inapasa kubadili jinsi inavyoshughulikia virusi vya corona ili kumaliza hali ambapo wananchi wanaona ugonjwa huo kama uhalifu ama hukumu ya kifo,” akasema Bw Gibore.
Kumekuwepo na ongezeko la watu wanaowekwa kwenye karantini kwa lazima wanapokamatwa na polisi kwa kutotii kanuni kama vile kuvaa maski, kukiuka kafyu, kukusanyika ama kusafiri nje ya maeneo yaliyopigwa marufuku.
Mnamo Jumatano, watu 57 waliwekwa kwenye karantini ya lazima katika Taasisi ya Mafunzo ya Matibabu (KMTC) mjini Meru kwa kupatikana wakitembea bila maski, kukaribiana sana na kusafiri kutoka Nairobi.
Katika Kaunti ya Nakuru, vijana 21 waliwekwa kwenye karantini walipopatikana karibu na Nakuru Golf Club wakiwa hawazingatii kanuni za serikali kuhusu Covid-19.
Katika misako dhidi ya wanaovunja sheria, polisi wamelaumiwa kwa kuwarundika washukiwa kwenye magari baadhi wakiwa hawana maski, na pia wao wenyewe kukosa kuzingatia kanuni hizo.
Kumekuwepo na visa pia ambapo watu ambao wamekubaliwa kuwa nje wakati wa kafyu ama kusafiri kutoka kaunti zilizofungwa wamekamatwa na kuwekwa kwenye karantini ya lazima.
Wanaowekwa kwenye karantini kwa lazima wanalazimika kulipia gharama za kukaa huko kwa siku 14, malipo ya chini yakiwa ni Sh2,000 kila siku.
Hapo jana maafisa wawili wa polisi walikuwa miongoni mwa watu 17 ambao wamewekwa karantini ya lazima katika Kaunti ya Nyandarua.
Kamishna Boaz Cherutich alisema wawili hao walipatikana pamoja na watu wengine wakinywa pombe ndani ya baa moja katika mji wa Maili Kumi.
Awali, watu wengine tisa waliwekwa karantini walipopatikana katika baa moja eneo la Mirangine.
“Watu 17 wamewekwa karantini ya lazima katika shule ya Nyandarua High kwa gharama yao wenyewe,” akasema Bw Cherutich.