Katibu Mkuu wa UN, Guterres alaani mauaji ya wanajeshi wa kulinda usalama Sudan
MKUU wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres amelaani shambulio lililotekelezwa kwa kutumia droni katika kituo cha umoja huo kilichoko Kadugli, nchini Sudan na kuwaua walinda usalama sita wa asili ya Bangladesh huku wengine wanane wakijeruhiwa.
Waaathiriwa walikwua wakihudumu kama kikosi kwa jina, “UN Interim Security Force for Abyei-UNISFA” kinacholinda usalama katika eneo linalobishaniwa la Abyei.
Kwenye taarifa Jumapili, Desemba 14, 2025 kupitia mtandao wa kijamii wa X Guterres alitaja shambulio hilo kama “baya zaidi” akiongeza kuwa wafanyakazi wa UN hawafai kushambuliwa kwani hatua hiyo inaweza kuchukuliwa kama uhalifu wa kivita chini ya sheria ya kimataifa.
“Kushambuliwa kwa walinda amani wa umoja wa mataifa kama ilivyofanyika Jumapili hakukubaliki na sawa na uhalifu wa kivita. Nakumbusha kila mmoja kuhusu wajibu wao wa kulinda maafisa wa umoja wa mataifa na raia. Kutahitajika kuwe na uwajibikaji,” akasema.
“Natoa rambirambi zangu kwa familia za wanajeshi waliouawa, serikali na watu wa Bangledesh. Nawatakia afueni ya haraka waliojeruhiwa,” Bw Guterres alieleza kwenye taarifa ikithibitisha kisa hicho.
Bangladesh imetoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuhakikisha usalama wa vikosi vya kulinda usalama na utunzaji kwa wanajeshi waliojeruhiwa.
“Serikali kupitia ubalozi wake katika Umoja wa Mataifa iliomba umoja huo kuhakikisha kuwa wanajeshi waliojeruhiwa wanapata matibabu bora zaidi,” ikasema Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Bangledesh.
“Afisi ya Ubalozi wa Bangladesh jijini New York inawasiliana na Umoja wa Mataifa na inajizatiti kutoa usaidizi kwa kikosi cha wanajeshi wa kulinda usalama wa asili ya Bangladesh walioko Sudan,” ikaongeza.
Jeshi la Sudan limedai kuwa shambulio hilo la droni lilitekelezwa na wapiganaji wa kundi la waasi la Rapid Support Forces (RSF) ambao wamekuwa wakiendeleza mashambulio sehemu kadhaa nchini humo.
RSF, inayoongozwa na Mohamed Hamdan Dagalo, ambaye pia anajulikana kama “Hemedt”, imekuwa ikipigana na Jeshi la Ulinzi la Sudan (SAF) tangu Aprili 2023 kuhusu udhibiti wa asasi za kijeshi na kisiasa nchini humo.
Mapigano hayo yameenea katika maeneo kadhaa, ikiwemo Darfur, Kordofan na Khartoum na kusababisha vifo vya maelfu ya watu huku mamilioni ya wengine wakifurushwa makwao.
Makundi ya kuteteta haki yamenakili visa kadhaa vya ukiukaji haki za kibinadamu na ukatili wakati wa vita hivyo, ikiwemo, mashambulio ya raia wasio na hatia na maeneo yaliyolindwa.
Hali hiyo imeibua hofu kuwa baadhi ya vitendo hivyo vinaweza kuchukuliwa kama uhalifu wa kivita.
Licha ya mataifa ya kimataifa kuhimiza usitishaji vita, mapigano nchini Sudan yameendelea kushika kasi hali inayowaweka hatarini raia na wafanyakazi wa mashirika ya kutoa msaada wa kibinadamu.