Kaunti bora kwa uwekezaji zafichuliwa
KAUNTI za Nairobi, Kiambu, Nyeri na Murang’a ndizo zimeibuka bora zaidi kuwekeza nchini Kenya, kwa mujibu wa utafiti mpya uliofadhiliwa na Umoja wa Ulaya kupitia shirika la Trademark Africa.
Ripoti hiyo, inayojulikana kama County Competitiveness Index (CCI), ni ya kwanza kutolewa nchini na inaonyesha ni kaunti zipi zilizo na mazingira bora zaidi kwa wawekezaji, ikizingatia vipengele kama ubora wa miundombinu, huduma za afya, usalama, na ukuaji wa uchumi wa ndani.
Kwa kutumia tafiti na takwimu za serikali, ripoti hiyo inachambua masuala kama uwepo wa taasisi za serikali, kiwango cha usalama wa umma, ukuaji wa uchumi wa kaunti, ajira, ubora wa miundombinu, elimu, mazingira ya biashara, na usimamizi wa mazingira.
Kiwango cha ushindani cha kila kaunti kilionyeshwa kwa asilimia, kikielezea uwezo wa kaunti kuunda mazingira bora ya biashara na kuvutia wawekezaji katika ngazi za ugatuzi.
Kaunti ya Nairobi iliongoza kwa ushindani ikiwa na asilimia 71, ikifuatiwa na Kiambu (asilimia 73), Nyeri (asilimia 61), Murang’a (asilimia 61), Nakuru (asilimia 57), Machakos (asilimia 56), na Mombasa ( asilimia 53).
Kaunti nyingine zilizo juu ya kiwango kinachokubalika cha asilimia 50 ni Kirinyaga (asilimia 52), Embu (asilimia 51), na Tharaka Nithi (asilimia 50).
Ripoti ilisema kaunti hizi zinaonyesha utendaji bora katika nyanja muhimu kama maendeleo ya kiuchumi, miundombinu na utawala bora.
Kaunti zilizopata alama za chini zaidi ni Wajir (asilimia 13), Tana River (asilimia 14), Garissa (asilimia 15), Marsabit (asilimia 16), na Mandera ( asilimia 17).
Utafiti unasema kaunti hizi zinakabiliwa na changamoto sugu katika miundombinu, wafanyakazi, na shughuli za kiuchumi. Kaunti nyingine zote zilipata kati ya asilimia 20 na 50.
Waziri wa Biashara na Uwekezaji, Lee Kinyanjui, alisema matokeo hayo yatasaidia wawekezaji wanaotafuta fursa nchini na pia kuongoza serikali za kaunti kuboresha mvuto wao wa uwekezaji.
“Tunaamini kwamba kwa mwekezaji yeyote, uamuzi kuanzia katika hatua ya kuchunguza hadi kuwekeza unategemea upatikanaji wa taarifa sahihi. Kukosekana kwa taarifa kunaweza kuwazuia kufanya maamuzi kamili,” alisema Bw Kinyanjui.
Ripoti hiyo imetolewa kabla ya utafiti mwingine wa Mamlaka ya Uwekezaji Kenya (KenInvest) ambao unatarajiwa kufichua kaunti 17 ambazo hazijawahi kupata uwekezaji mkubwa tangu kuanza kwa ugatuzi miaka 12 iliyopita.
Ripoti ya kwanza ya CCI imependekeza kaunti kuimarisha utawala na uwezo wa taasisi, kupanua miundombinu na ushirikiano wa kanda, na kuwekeza katika ujuzi wa wakazi kikazi ili kuongeza ushindani wao.
Pia imependekeza mageuzi makubwa kuboresha ufanisi wa biashara, utekelezaji wa mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na maendeleo katika kaunti zenye uwezo duni wa kuvutia wawekezaji.
Ripoti hiyo ilibaini kwamba kaunti zilizopata alama za juu kwa kawaida zina taasisi imara, usalama wa kutosha, uwepo mkubwa wa serikali, uchumi unaokua kwa kasi, na miundombinu iliyoimarishwa.
“Hii inaonyesha kuwa mifumo imara ya taasisi, shughuli thabiti za kiuchumi, na miundombinu iliyoboreshwa ndizo nguzo kuu za ushindani mkubwa,” utafiti ulisema.
Kwa upande mwingine, kaunti zilizo na ushindani mdogo kama Wajir, Tana River, Mandera, na Garissa zina upungufu mkubwa katika elimu, afya, miundombinu na utawala.
“Kaunti zisizo na ushindani zinapaswa kuanza kwa kuwekeza katika huduma za msingi kama maji, elimu na afya ili kuziba pengo la maendeleo ya kimsingi,” utafiti huo ulipendekeza.