Habari

Kenya sasa ina visa 4 vya Covid-19

March 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Afya Mutahi Kagwe amethibitisha kisa kingine cha mgonjwa wa COVID-19.

Akihutubia wanahabari Jumanne katika Afya House, amesema mgonjwa huyo aliwasili nchini Machi 9, 2020, kutoka Uingereza.

Amezungumzia pia kuhusu watu waliokuwa katika hospitali ya Mbagathi wakichunguzwa kuhusu afya zao na kuhusu COVID-19.

“Watu 23 waliokuwa katika karantini hospitalini Mbagathi wameruhusiwa kuenda nyumbani baada ya vipimo kubainisha hawana COVID-19,” amesema Waziri Kagwe akiwataka wajitenge binafsi kila mmoja.

Waziri amesema vipimo vilivyofanyika nchini kufikia sasa ni 111 ambapo 71 matokeo yalionyesha hakuna COVID-19 huku 36 vikiendelea kuchunguzwa na vinne vikionyesha maambukizi ya COVID-19.

Kufikia sasa Kenya ina jumla ya visa vinne.

Kisa cha kwanza kilitangazwa Ijumaa wiki jana huku vingine viwili vikitangazwa Jumapili.