Habari

Kenya yathibitisha visa saba vipya vya Covid-19

March 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY WAWERU

KENYA imethibitisha visa saba vipya vya Covid-19 idadi jumla ikifika 38, amesema Waziri wa Afya Mutahi Kagwe akihutubia wanahabari katika Afya House jijini Nairobi Jumamosi mchana.

Waziri Kagwe amesema visa hivi vipya ni vya wagonjwa walio jijini Nairobi, hali inayofanya kaunti hii kuongoza ikiwa na visa 28.

Kaunti zingine ambazo tayari zina visa vya maambukizi ya virusi vya corona ni Kilifi (6), Mombasa (2) na Kajiado na Kwale zilizo na kisa kimoja kila moja.

Kagwe amesema idadi hiyo ya visa vipya imebainika baada ya sampuli kutoka kwa watu 81 kuchukuliwa na kufanyiwa vipimo.

“Wakenya ni wanne, wawili raia wa Congo na raia mmoja wa China,” ameeleza Bw Kagwe.

Kati ya saba hao, wagonjwa wanne ni wa kiume watatu wakiwa jinsia ya kike.

Waziri pia amesema mgonjwa wa pili aliyetangazwa kupata nafuu, vipimo zaidi vimethibitisha amepona kabisa na kwamba ameruhusiwa kuondoka hospitalini.

“Vipimo vya mgonjwa wa kwanza na wa tatu, vimeonyesha matokeo hasi kumaanisha hawana virusi hivyo tena. Hata hivyo, tunasubiri kuwathibitisha kwa vipimo vingine zaidi kwa muda wa saa 48 zijazo,” amefafanua.

Kaunti ya Nairobi imetajwa kama iliyoathirika pakubwa kwa Covid-19, ikiongoza kwa wagonjwa 28. Kaunti zingine zilizoathirika ni pamoja na Mombasa, Kilifi na Kwale.

Waziri Kagwe amesema jumla ya watu 883 wamekaguliwa na kufanyiwa vipimo vya virusi vya corona, huku zaidi ya 1,000 wakisemekana kutangamana na wagonjwa.

“Ikibainika ulitangamana na mgonjwa maafisa wa idara ya afya kwa ushirikiano na wale wa usalama watakuja kwako, wakuchukue ili upitie karantini ya lazima,” amesisitiza Waziri.

Waziri amewataka Wakenya wawe makini na wazingatie utaratibu uliowekwa kuhusu umbali wanaofaa kukaa – mtu akiwa na mwenzake au wenzake – ili kuepuka maambukizi.

“Mtazame kwa makini mtu aliye kando yako; huyo mtu anaweza kuwa na virusi vya corona,” amesema Kagwe.