Habari

KERO LA KRISMASI: Ajali, ndoa kuyumba, maradhi na ulevi huku Ukimwi ukisambazwa zaidi

December 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 3

Na VALENTINE OBARA

WAKENYA wengi Krismasi hii watajumuika na jamaa na marafiki kwa sherehe sawa na ilivyo katika mataifa mengine mengi ulimwenguni.

Hata hivyo, sherehe hizi zimekuwa zikiandamana na mambo yenye madhara kwa watu kibinafsi na kwa jamii yote kwa misingi mbalimbali ikiwemo afya, mahusiano kuvunjika, vifo vinavyoweza kuepukika kama vile kupitia ajali na fujo zinazosababishwa na ulevi.

Kwa kutambua matatatizo yanayoandamana na Krismasi, Rais Uhuru Kenyatta hapo Jumatatu kwenye ujumbe wake wa heri njema za Krismasi aliwashauri Wakenya kujihadhari wakati wa sherehe ili wasiweke maisha yao hatarini.

“Mnaposherehekea na jamaa na marafiki msimu huu, ninawaomba Wakenya wote kuwajibika wanapofanya hivyo,” akasema Rais Kenyatta.

 

Ndoa kuingia doa

Kulingana na utafiti uliofanywa na wasomi kutoka Chuo Kikuu cha Washington nchini Amerika, ndoa nyingi huvunjika mara baada ya Krismasi. Wanasayansi hao, Profesa Julie Brines na Brian Serafini, wanasema shinikizo za sherehe za Krismasi zinaweza kuathiri ndoa, hasa iwapo matarajio ambayo familia huwa nayo yatakosa kutimia.

“Krismasi huwa msimu ambapo kunakuwa na matarajio ya kupata mwanzo mpya katika ndoa. Matumaini hayo yakikosa kutimia kunazuka mivutano ya kifamilia na kuvunjika moyo kwa wanandoa, hali inayopelekea wengi kuachana,” wakasema.

Pia wanasema masuala ya fedha wakati wa Krismasi huchangia hali hiyo. Hii ni kutokana na mazoea ya wengi kutumia pesa kiholela kusherehekea, na mara baada ya sikukuu wanaanza kuhangaika, hali inayozua mizozo ya kifamilia.

Tabia ya wengi kusherehekea kupindukia hasa kwa kulewa pia imetajwa kama kishawishi cha wengi kushiriki ngono kiholela, suala ambalo ni tishio kwa ndoa na mahusiano mengine ya kimapenzi.

Mtaalamu wa masuala ya familia na malezi Bi Liz Wanyoike anakubaliana na utafiti huo akisema matukio mengi wakati wa Krismasi yakiwemo ya kiuchumi, watu kutangamana zaidi, ngono kiholela na anasa kupindukia ndizo sababu kuu za ndoa kuathirika kutokana na Krismasi hapa Kenya.

 

Ajali

Kulingana na Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama na Uchukuzi (NTSA) na Idara ya Polisi, ajali za barabarani nazo huongezeka wakati wa msimu huu kila mwaka kwa sababu ya jinsi safari zinakuwa nyingi watu wakisafiri maeneo mbalimbali.

Kwa karibu wiki mbili sasa, ajali nyingi zimeripotiwa mijini na katika barabara kuu sehemu mbalimbali za nchi ikiwemo zinazohusisha magari ya kibinafsi na watu kadhaa wamepoteza uhai

Mkurugenzi Mkuu wa NTSA, Bw Francis Meja, alisema Jumatatu kuwa ongezeko la safari humaanisha magari yataongezeka barabarani, kwa hivyo misongamano inatarajiwa, hivyo basi wanaotaka kuwasili wanakoenda mapema waanze safari mapema badala ya kuendesha magari kwa kasi.

“Ongezeko la safari pia husababisha wahudumu wa magari mengi ya uchukuzi wa umma kusafiri katika barabara ambazo hawajaidhinishwa. Tunawaomba Wakenya wasiabiri magari ambayo hayajaidhinishwa kuhudumu maeneo wanakoelekea,” akasema.

Mbali na ajali, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limetoa tahadhari kuhusu aina ya vyakula maarufu wakati wa sherehe, vinavyoweza kusababisha gharama kubwa za kutafuta matibabu 2019 na baadaye kutokana na matatizo ya afya.

 

Magonjwa

Magonjwa kama vile maradhi ya moyo, kiharusi, saratani, ongezeko la uzani kupita kiasi, na matatizo ya ini hutokana na ulaji wa vyakula na kunywa vinywaji vyenye kiwango kikubwa kupita kiasi cha mafuta, chumvi, sukari na unywaji wa pombe kupita kupindukia.

“Kile tunachokula na kunywa kinaweza kuathiri uwezo wa miili yetu kukabiliana na magonjwa, na pia huamua kama tutakumbwa na matatizo ya kiafya baadaye maishani ikiwemo uzani mkubwa kupita kiasi, magonjwa ya moyo na aina mbalimbali za saratani,” WHO ikaeleza kwenye ripoti yake.

 

Pombe

Madhara ya pombe huwa si ya kiafya pekee, bali imethibitishwa kuwa chanzo cha ajali, mizozo ya kifamilia na kuongezeka kwa maambukizi ya magonjwa ya zinaa ikiwemo Ukimwi kutokana na ngono kiholela.

Visa vya uhalifu navyo huongezeka hasa mijini wakati wakazi wanaposafiri kuelekea sehemu zingine za nchi, ambapo wezi hutumia fursa hii kuvunja nyumba. Wahalifu pia huongeza bidii ili kupata pesa za kusherehekea sikukuu sawa na Wakenya wengine.

Inspekta Mkuu wa Polisi Joseph Boinnet, hivi majuzi aliwahakikishia Wakenya kuwa usalama utadumishwa kote nchini.

Alisema usalama utazidishwa katika maeneo muhimu kama vile makanisani na sehemu za burudani ili kuzuia visa vya uhalifu.