Habari

Kibaki awekea Uhuru presha

June 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

MAFANIKIO ya maendeleo aliyopata Rais Mstaafu Mwai Kibaki katika utawala wake wa miaka 10 ndiyo yamempatia presha Rais Uhuru Kenyatta kujaribu kuacha sifa njema atakapostaafu 2022, duru zimedokeza.

Licha ya kuwa amebakisha miaka miwili pekee kwenda nyumbani, duru katika kundi la wandani wa kiongozi wa taifa zimeeleza kuwa ghafla Rais Kenyatta ametambua huenda akastaafu akiwa na sifa mbaya hasa anakotoka Mlima Kenya, ambako wengi wanahisi amewavunja moyo.

Taifa Leo imedokezewa kuwa hiki ndicho kiini cha Rais kuwateua kwenye vyeo vikuu watu wa jamii za Mlima Kenya walio waaminifu kwake kusimamia wizara na idara kubwa kubwa ili angaa kuona kama atatimiza Ajenda Nne za Maendeleo.

“Ghafla Rais amegundua atastaafu kama Rais hafifu akilinganishwa na Mwai Kibaki ambaye sifa zake zimejaa kitaifa na Mlima Kenya kwa maendeleo aliyoafikia,” akasema mmoja wa wahusika katika mikakati ya kuokoa sifa za Rais Kenyatta.

Akaongeza: “Rais ameamua kuchukua tena usukani Mlima Kenya. Anajua kuwa eneo hilo ndilo litakuwa na uamuzi wa ni nani atakayekuwa Rais 2022 kutokana na kura zake nyingi. Hivyo lazima amalize ushawishi mkubwa wa Naibu Rais William Ruto mashinani.”

Wizara kubwa zinazohusika na Ajenda Nne zinasimamiwa na watu kutoka Mlima Kenya. Hizi ni Kilimo (Peter Munya), Afya (Mutahi Kagwe) na Uchukuzi na Nyumba (James Macharia).

Rais pia anatumia mbinu ya kuhakikisha amechukua usukani katika Seneti na Bunge ili miswada anayohitaji ipitishwe kwa urahisi.

“Ni lazima Rais afanye kazi na watu waaminifu kwake ili wamsaidie kutimiza ajenda zake,” Seneta Irungu Kang’ata wa Murang’a akaambia Taifa Leo.

Kuteuliwa kwa Bw Kang’ata kuwa Kiranja wa Wengi katika Seneti kulitokana na uwezo wake wa kushawishi vijana mashinani hasa katika Kaunti za Kiambu na Murang’a.

Nao uteuzi wa Mbunge wa Kipipiri Amos Kimunya kuwa Kiongozi wa Wengi kumedokezwa pia kuwa sehemu ya mikakati ya Rais ili aweze kusukuma ajenda zake bungeni kutokana na uaminifu wake na ujuzi aliopata alipokuwa waziri katika utawala wa Mzee Kibaki.

Bw Kimunya pia ana uhusiano wa karibu na wafanyibiashara wakubwa wa Mlima Kenya na anatarajiwa kumsaidia Rais hasa katika kushawishi wakulima wa viazi, kahawa, chai na maziwa kuunga mkono ajenda za Rais Kenyatta na kuongoza kampeni ya siga zake Nyandarua na Nakuru.

Katika kuhakikisha kuwa migao ya fedha anayotaka imepita kwa urahisi bungeni, Mbunge wa Kieni Kanini Kega anatarajiwa kuteuliwa kuchukua mahala pa Kimani Ichung’wa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti bungeni.

Bw Kega pia amepewa kibarua cha kuridima ngoma ya Rais Kenyatta katika kaunti za Nyeri na Laikipia.

Duru zinadokeza Rais pia yupo makini kuhakikisha Mbunge wa Kangema, Muturi Kigano ameteuliwa mwenyekiti wa Kamati ya Sheria bungeni ili aweze kusukuma ajenda ya BBI.

Ingawa BBI imepokelewa kwa ubaridi Mlima Kenya, Bw Kang’ata anasema nakala inayoandaliwa itabadilisha mambo.

“BBI itapokelewa kwa wingi Mlima Kenya baada ya kifungu cha ugawaji fedha kulingana na idadi ya watu kuwekwa. Hii inatarajiwa kushawishi wakazi kuiunga mkono kwani watafaidika pakubwa kuliko wengine,” akasema Bw Kang’ata.

Spika wa Bunge la Taifa Justin Muturi naye ni muhimu katika kutimiza matakwa ya Rais Kenyatta kwa bunge pamoja na kushawishi wakazi wa Embu, huku Naibu Kiranja wa Wengi Maoka Maore akitegemewa Meru na Tharaka Nithi.