Habari

Kigame atoa wito vijana wajisajili kama wapiga kura

Na WINNIE ONYANDO October 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MSANII maarufu wa nyimbo za injili Reuben Kigame ambaye pia ana nia ya kuwania kiti cha urais 2027 ametoa wito kwa Wakenya kujisajili kama wapiga kura na kujitokeza kwa wingi wakati wa uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza jana katika Kituo cha Ufundi na Burudani cha Velndale Dandora, Dkt Kigame alithibitisha kuwa uchaguzi ujao utakuwa tofauti kwani vijana wako tayari kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa wazi.

“Usife moyo au kukata tamaa ukifikiri kura yako haitahesabiwa kwa sababu naamini wakati huu, itakuwa vigumu kuiba kura zetu kwa sababu tuna vijana wengi walio tayari kufuatilia kila kituo,” akasema Dkt Kigame.

Katika ziara hiyo ambapo alitoa misaada ya cherehani, unga na sukari kwa wanafunzi katika taasisi hiyo, Dkt Kigame alisema kuwa kutimiza ahadi ni thamani anayoizingatia, akisema “Ni bora kutoahidi kuliko kuahidi na kutotimiza.”

“Hatuna mabilioni ambayo wengine wanayo, lakini tunatoa kidogo tulichonacho,” Kigame alisema.

Mkewe, Julie Kigame ambaye pia alihudhuria hafla hiyo alisema kuwa, “Siku zote Dkt Kigame yuko tayari kuwatumikia wananchi.”

Rais wa kituo hicho, Justus Ezekiel na mkuu wa ustawi wa jamii Faith Wangui wote walimsifu Kigame kwa kutimiza ahadi yake wiki moja tu baada ya kutoa ahadi hiyo.

“Tuliomba cherehani, na alituletea zaidi ya hiyo. Tunashukuru.”