Adani aitwa Amerika kujibu kesi ya ufisadi
TUME inayosimamia Soko la Hisa nchini Amerika (SEC) imemuita bilionea Gautam Adani, aliyeshtakiwa juzi kwa ufisadi kujibu kesi, stakabadhi za mahakama zilionyesha.
SEC imemshtaki mmiliki na mwenyekiti huyo wa kundi la Kampuni za Adan, na mpwa wake Sagar Adani ikidai walipeana mamilioni ya dola kama hongo ili kuisaidia mojawapo ya kampuni zake kupata zabuni India.
Tume hiyo inadai Adani alihadaa kuwa kampuni yake huzingatia sheria za kupambana na rushwa wakati wa ununuzi wa hisa za thamani ya dola 750 milioni (Sh96.8 bilioni).
Ilani hiyo ya kumuita kujibu mashtaka inahitaji kujibiwa ndani ya siku 21 kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa Jumatano katika mahakama jijini New York.
Tume ya SEC inataka korti itoe adhabu ya pesa na iwazuie wawili hao kuendelea kuwa maafisa wa kampuni zilizosajiliwa katika soko hilo la hisa.
Wawakilishi wa Adani Group jana hawakujibu shirika la habari la Reuters liliposaka maoni yao kuhusu suala hilo.
Kampuni hiyo imekana mashtaka hayo ikidai hayana “msingi wowote”.
Afisa Mkuu wa Masuala ya Kifedha katika Adani alisema shtaka hilo linahusiana na kandarasi moja ya kampuni ya Adani Green Energy ambayo ni asilimia 10 ya biashara yake, na kwamba hamna kampuni nyingi katika kundi hilo imepatikana na makosa yoyote.
Imetafsiriwa na Charles Wasonga
.