Afisa wa Muslim Brotherhood afariki gerezani
Na MASHIRIKA
CAIRO, MISRI
AFISA wa cheo cha juu wa kundi lililoharamishwa la Muslim Brotherhood amefariki akiwa katika gereza hatari la Tora jijini Cairo baada ya kukumbwa na mshtuko wa moyo, maafisa wa usalama wa Misri wamesema.
Essam el-Erian, ambaye alikuwa amehukumiwa kufungwa jela mara kadhaa kufuatia mapinduzi ya serikali ya kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri, alifariki akiwa na umri wa miaka 66.
El-Erian alikuwa amehamishiwa hospitali ya gereza baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo na alikufa akiendelea kutibiwa, maafisa wawili wa gereza walisema.
Msemaji wa Muslim Brotherhood, Abdel Moneim alisema kwamba wakuu wa magereza waliwafahamishwa kuwa kifo cha El- Erian kilikuwa cha kawaida.
Alisema kwamba alipokea simu kutoka kwa wakuu wa gereza Jumatano kumfahamisha kuhusu kifo cha el-Erian.
“Sijui iwapo alifariki akiwa gerezani au akiwa hospitalini,” aliambia shirika la habari la Anadolu.
“Nilifahamisha familia yake kuhusu kifo chake ili ianze kuandaa mipango ya mazishi,” alisema.
Kulingana na Abdul-Maqsoud, yeye na familia ya el-Erian hawakuwa wamemuona kwa miezi sita baada ya serikali kusimamisha ziara katika magereza kama hatua ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.