Kimataifa

Aibu Rwanda ikikubali kupewa wahamiaji haramu kutoka Amerika

Na MASHIRIKA August 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIGALI, RWANDA

RWANDA ni taifa la hivi punde ambalo limekubali kuwapokea wahamiaji haramu kutoka Amerika.

Nchi hiyo ilitangaza kuwa itawapokea wahamiaji 250 kutoka Amerika ili nayo inufaikie ukarimu wa fedha kutoka kwa utawala wa Rais Donald Trump.

Imebainika kuwa mkataba huo ulitiwa saini jijini Kigali mnamo Juni kwa mujibu wa mmoja wa afisa wa ngazi ya juu kutoka serikali ya Rwanda.

Amerika imekuwa ikiafikia mkataba na nchi zenye uchumi mdogo ili kuwapokea wahamiaji haramu ambao wengi wao ni wahalifu sugu wanaotumikia vifungo vya aina mbalimbali nchini humo.

“Rwanda imekubali kuwapokea wahamiaji haramu 250 kutoka Amerika. Hii ni kwa sababu Rwanda ni kati ya mataifa ambayo yamekumbana na uhamiaji na tamaduni yetu imejikita katika uwiano,” akasema Msemaji wa Serikali ya Rwanda Yolande Makolo.

“Chini ya makubaliano hayo, Rwanda itakuwa na nafasi ya kushauriana na kila mhamiaji. Wale ambao wataidhinishwa watapewa mafunzo, huduma za afya na makazi ili wayaanze maisha yao mapya Rwanda. Hii itawapa nafasi ya kuchangia uchumi wa nchi unaokua kwa haraka duniani,” akaongeza.

Ikulu ya White House hata hivyo, bado haikuwa imezungumzia suala hilo. Mbali na Rwanda, Sudan Kusini na Eswatini ni nchi nyingine za Afrika ambazo zimewapokea wahamiaji haramu kutoka Amerika.

Licha ya kukubali kuwapokea wahamiaji hao, maswali yameibuliwa kuhusu iwapo Rwanda inazingatia haki na itawashughulikia kwa kuzingatia haki za kimataifa.

Utawala wa Rais Trump umekuwa ukisisitiza kuwa nchi zenye uchumi mdogo zitasaidia katika kupunguza idadi ya wahamiaji wakiwemo wahalifu sugu Amerika.

Idara ya uhamiaji Amerika inaona nchi zenye uchumi mdogo kama hifadhi za wahalifu sugu ambao ni tishio kwao na si rahisi kuwarejesha kwao.

Ingawa hivyo, kumekuwa na hofu kuwa watu kutupwa nchi wasizozipenda ni hatari kwa sababu watakumbana na uadui, hawana uhusiano wowote wa kidamu na kulemewa kuzungumza lugha kwenye taifa la jipya.

Kwa kuwapokea wahamiaji hao, Rwanda italipwa japo bado haijajulikana ni pesa kiasi gani.

Duru zinaarifu kuwa idadi ya wahamiaji ambao watapelekwa Rwanda nayo pia itaongezwa lakini kupitia maelewano kati ya nchi hizo mbili.

Utawala wa Trump umekuwa ukishinikiza mataifa mengi yakubali kuwapokea wahamiaji kisha unawapa pesa.

Mnamo Machi, Amerika iliwapeleka zaidi ya wahamiaji 200 Venezuela na ilidaiwa wahamiaji hao walikuwa wahalifu sugu waliokuwa wamekamilisha vifungo vyao.

Viongozi wa Magharibi na Afrika wamekuwa wakimsifu Rais Paul Kagame kwa kugeuza na kuyatekeleza mabadiliko makubwa Rwanda tangu mauaji ya halaiki mnamo 1994.

Pia Rwanda imekuwa ikishiriki mazungumzo na Amerika kuhusu kupatikana kwa amani ya kudumu mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Hii si mara ya kwanza Rwanda inakubali kuwapokea wahamiaji.

Mnamo 2022 ilitia saini mkataba na Uingereza ili kuwapokea maelfu ya raia waliokuwa wakisaka makao.

Hata hivyo, mkataba huo uliondolewa hata kabla ya kutekelezwa na Waziri Mkuu mpya Keir Starmer.

Hakuna mtu alisafirishwa Rwanda kwa sababu suala hilo pia lilipingwa kortini Uingereza.