Kimataifa

Ajabu kampuni maarufu ya sigara kutaka wateja waache uvutaji

October 23rd, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA AFP

MOJAWAPO ya kampuni kubwa za kutengeneza sigara duniani, Philip Morris, imeshangaza wateja wake baada ya kuandaa matangazo na kampeni ya kuwahimiza kuachana na uvutaji wa sigara ili kuepuka maradhi ya kansa.

Kampuni hiyo inayotengeneza sigara za ‘Marlboro’ ilisema kuwa tangazo hilo ni moja ya hatua ambazo imechukua katika harakati za kutaka kuacha uuzaji wa sigara.

Lakini Taasisi ya Kutafiti Saratani nchini Uingereza imekosoa hatua ya kampuni hiyo huku ikisema kuwa hiyo ni njama ya kutangaza sigara yake mpya ya kielektroniki.

Sigara ya kielektroniki hupasha joto tumbaku na kutoa mvuke uliosheheni nikotini. Hiyo ni tofauti na sigara ya sasa ambapo waraibu wake huchoma tumbaku na kubugia moshi ulio na kemikali ya nikotini.

“Huu ni unafiki,” ikasema taasisi hiyo huku ikisema kuwa kampuni ya Philip Morris bado inapigia debe sigara zake za Marlboro nje ya Uingereza.

“Ikiwa kampuni ya Philip Morris inataka watu wasivute sigara basi ikome kuzitengeneza,” akasema George Butterworth, meneja wa sera katika Taasisi ya Kutafiti Kanasa nchini Ungereza.

Taasisi hiyo ilisema kwamba uvutaji wa sigara ni miongoni mwa visababishi vikubwa vya maradhi ya saratani.

Shirika linaloendesha kampeni dhidi ya uvutaji wa sigara, Action on Smoking and Health (Ash), pia limekosoa vikali kampuni ya Philip Morris kutokana na kile lilitaja kuwa unafiki.

Katika tangazo lake la video, kampuni ya Philip Morris, inaonyesha mwanamke akitupa kiberiti cha kuwashia sigara kama ishara kwamba ameachana na uvutaji wa sigara.

Serikali ya Uingereza imepiga marufuku matangazo ya kupigia debe uvutaji wa tumbaku na sigara zinazouzwa katika pakiti zisizo na maandishi.

Deborah Arnott, mkurugenzi wa Ash, alishutumu kampuni ya Philip Morris kwa unafiki huku akisema kuwa bado inapigia debe, kupitia matangazo, katika mataifa ambapo matangazo ya sigara hayajapigwa marufuku.

“Kampuni ya Philip Morris inatangaza sigara zake za Marlboro kichinichini huku ikijifanya kwamba inaendesha kampeni ya kuhimiza watu kuachana na uvutaji wa tumbaku,” akasema.

Hata hivyo, kampuni ya Philip Morris imeshikilia kuwa inalenga kuhakikisha kwamba wateja wake wanaachana na uvutaji wa sigara katika siku za usoni.

Mbali na sigara za Marlboro, kampuni ya Philip Morris hutengeneza sigara za kielektroniki kama vile Nicocig, Vivid na Mesh.

Mkurugenzi wa Philip Morris, Peter Nixon alisema kwamba kampuni hiyo inalenga kuacha utengenezaji wa sigara lakini alisisitiza kuwa ‘hilo litachukua muda mrefu kuafikiwa’.