Aliyefungwa kwa kuua mtoto auawa na mahabusu mwenzake seli
MASHIRIKA Na PETER MBURU
MWANAUME aliyetupwa jela kwa kumuua mtoto wa miaka minane amedaiwa kuuawa na mahabusu waliyefungwa katika seli moja, katika jela ya Oklahoma, Amerika.
Ripoti kutoka jela hiyo zilisema kuwa afisa wa polisi wa jela hiyo alipata mwili wa Anthony Joseph Palma wa miaka 59 mwendo wa saa moja na nusu Ijumaa jioni wakati wa kukagua jela. Ilisemekana kuwa juhudi za kumrejesha uhai mfungwa huyo hazikufua dafu na saa moja baadaye akadhibitishwa kufa.
Hata hivyo, habari kuhusu namna aliaga dunia wala mfungwa mwenza wa seli hiyo hazikutolewa, japo alielezwa kuwa alikuwa akihudumu kifungo cha mauaji, shirika moja la habari likasema.
Palma aliaga mwaka mmoja baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha gerezani, kwa mauaji ya Kirsten Hatfield, mtoto wa miaka minane.
Ilisemekana kuwa mtoto huyo alitoweka mnamo 1997 alipokuwa nyumbani kwao, katika jiji la Midwest, Oklahoma.
Mamake alisema kuwa alimlaza saa tano na nusu adhuhuri lakini alipoenda kumwangalia jioni hakumpata.
Damu ilionekana katika dirisha la chumba cha kulala, kisha nguo ya mtoto huyo ya ndani ikapatikana nyumba ya nyumba.
Hata hivyo, mwili wake haukuwahi kupatikana.
Viongozi wa mashtaka walisema kuwa Palma ambaye alikuwa jirani ya familia hiyo alimteka nyara, akamnajisi kisha akamuua mtoto huyo, gazeti la The Oklahoman likasema.
Mnamo Oktoba 2015, jamaa huyo alikamatwa baada ya vipimo vya DNA kwenye dirisha la chumba cha kulala alimokuwa Kirsten na kwenye chupi iliyokuwa ya mtoto kuonyesha alikuwepo.
Jamaa huyo aliripotiwa kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na dadake mkubwa mtoto huyo, wakati mauaji hayo yalipotendeka.
Alipohojiwa wakati huo 1997 na pia 2015, Palma alishikilia kauli yake kuwa wakati wa tukio hilo, alikuwa nyumbani kwake.
Hata hivyo, mwezi mmoja baada yake kukamatwa, alijaribu kujiondoa uhai japo hakufanikiwa, ripoti zikasema.
Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa jamaa huyo kukinzana na sheria.
Mnamo 1982, aliyekuwa mwenye nyumba wake alimlaumu kuwa alimvuta na kumchapa katika mtaa wa Walters, Oklahoma.
Hii ilikuwa licha ya madai kuhusu hali yake kumdhulumu mtoto mwingine wa kike kati ya 1979 na 1980 katika mtaa huo wa Walters.