Amerika yamrudisha mlinzi wa enzi za Nazi kwao
BBC na PETER MBURU
MWANAMUME Mjerumani wa miaka 95 ambaye alishirikiana na utawala wa Nazi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia hatimaye amerejea katika nchi yake, baada ya kutimuliwa kule Amerika miaka 15 iliyopita.
Jakiw Palij amekuwa akiishi bila uraia wa nchi yoyote tangu jaji mmoja wa Marekani alipofutilia mbali uraia wake wa nchi hiyo mnamo 2003.
Kwa muda huo, Ujerumani nayo ilidinda kumpokea kwani hakuwa na uraia wao.
Alipofika eneo la Dusseldorf, Ujerumani ripoti zilisema alipelekwa katika makao ya wazee, huku balozi wa US huko Berlin, Richard Grenell akisifu serikali ya sasa ya Ujerumani kwa kusuluhisha kesi hiyo.
Kulingana na maafisa wa utawala, Jakiw Palij ndiye mwandani wa Nazi pekee aliyekuwa akiishi Marekani, na makao yake eneo la Queens, jijini Newyork yalivutia maandamano miongoni mwa wakazi.
Palij anasemekana kuzaliwa eneo la Poland ambalo sasa liko nchi ya Ukraine. Mnamo 1943, anasemekana kuhudhuria kambi ya mafunzo ya Trawnki SS wakati Poland ilikuwa himaya ya Nazi.
Kambi ya Trawnki iliogopewa kwa kutoa mafunzo kwa maelfu ya wananchi walioishia kuwa walinzi wa kambi hiyo ya vifo eneo la Sobibor, Treblinka na Belzec.
Mlinzi wake aliyeogopewa sana alikuwa John Demjanjuk ambaye alihukumiwa na mahakama ya Ujerumani kwa kuchangia vifo vya watu 28,000 eneo la Sobibor. Alitimuliwa US mnamo 2009.
Wayahudi walitumwa katika kambi wakati wa oparesheni iliyoitwa Reinhard, ambayo ulikuwa mpango wa wana Nazi kuua zaidi ya wayahudi milioni mbili.
Katika kambi hiyo ya Trawnki, zaidi ya wayahudi 6,000 waliuawa Novemba 3, 1943, huku habari kutoka ikulu ya White House Marekani zikisema jukumu alilochukua Bw Palij lilichangia vifo vya wayahudi moja kwa moja.
Alifika Marekani 1949 na akapewa uraia 1957. Yeye mwenyewe alikana kushirikiana na wanaNazi na mnamo 2003 alieleza gazeti la New York Times kuwa alikubali kuwafanyia kazi ili kuokoa familia yake isiuawe.
Utofauti wa kidiplomasia baina ya mataifa ya Marekani, Ukraine, Poland na Ujerumani kuhusu ni nchi gani haswa Bw Palij alitoka ulichelewesha kurejeshwa kwake, hata baada ya kutimuliwa Amerika mnamo 2003.