Kimataifa

Askofu kutumia helikopta kutimua mapepo jijini

July 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

MASHIRIKA Na PETER MBURU

ASKOFU wa Kikatoliki nchini Colombia ametangaza kuwa atatumia ndege kunyunyizia jiji moja maji matakatifu, ili kufurusha mapepo ambao anaamini wanalisumbua.

Monsignor Ruben Dario Jaramillo Montoya atafanya hivyo kwa kutumia helikopta ya kijeshi jijini Buenaventura wakati wa kuadhimisha siku ya watakatifu mwaka huu.

“Tunataka kuzunguka kote Buenaventura tukiwa angani na kumwaga maji matakatifu kuona ikiwa tutaondoa pepo wote ambao wanaharibu bandari yetu,” askofu huyo akaeleza kituo cha redio cha Colombia.

Askofu huyo ambaye aliteuliwa na Papa Francis mnamo 2017 alisema kuwa anataka kumaliza uovu wote ambao uko katika mitaa ya jiji hilo, katika zoezi hilo la helikopta.

Jiji la Buenaventura limekuwa likikumbwa na tatizo la ulanguzi wa mihadarati na fujo kutoka kwa makundi ya kihalifu.

“Tunafaa kumaliza huyu shetani ili tuone ikiwa tutarejesha utulivu ambao jiji limepoteza kutokana na hali ya uhalifu kuongezeka, ufisadi na ulanguzi wa dawa za kulevya,” akasema Montoya.

Alisema zoezi hilo litakuwa la umuhimu kwani litasaidia kumaliza mabaya hayo katika jamii ya huko.

Askofu huyo alisema kuwa hadi sasa, kumekuwa na visa 51 vya mauaji katika jiji hilo tangu mwaka ulipoanza.