Bashir atupwa kwa gereza alilokuwa akitupa waliompinga
WANDERI KAMAU NA MASHIRIKA
ALIYEKUWA rais wa Sudan, Omar Al Bashir, Jumanne alipelekwa katika gereza la wahalifu sugu alilotumia kuzuilia mahasimu wake wa kisiasa jijini Khartoum.
Bashir ambaye alipinduliwa na jeshi wiki iliyopita amekuwa akizuiliwa katika eneo lisilojulikana. Na jana, famili yake ilithibitisha kuwa amehamishiwa katika gereza la Kober.
“Usiku wa kuamkia jana, Bashir alipelekwa katika gereza la Kober, lililo jijini Khartoum,” akasema jamaa yake ambaye hakutaka kutajwa kutokana na sababu za kiusalama.
Bashir alipinduliwa mamlakani Alhamisi wiki iliyopita, baada ya maandamano makubwa dhidi ya utawala wake wa kiimla ambayo yalidumu kwa miezi minne.
Mara baada ya kupindua serikali yake, Baraza la Kijeshi ambalo sasa linaongoza nchi hiyo, lilisema kuwa Bashir alikuwa akizuiliwa “mahali salama.”
Walioshuhudia walisema kulikuwa na wanajeshi wengi nje ya gereza hilo, lililo kaskazini mwa Khartoum.
“Kulikuwa na wanajeshi waliokuwa wakishika doria nje ya gereza hilo wakiwa na magari yaliyokuwa na silaha kali,” akasema mtu mmoja.
Licha ya kuzuiliwa kwake, baadhi ya waandamanaji bado wanaeleza kutoridhishwa na hatua hiyo. Wamekuwa wakipiga kambi nje ya makao ya jeshi kwa siku kadhaa tangu kung’atuliwa kwake.
Utawala huo umejaribu kutimiza matakwa ya waandamanaji hao, baadhi yakiwa kufutwa kazi kwa aliyekuwa Kiongozi wa Mashtaka Omer Ahmed Mohamed.
Licha ya hatua hiyo, baadhi ya waandamanaji wanahofia kwamba huenda baadhi ya matakwa yao yakakosa kuzingatiwa.
“Tulirushiwa gesi ya kutoa machozi. Tulipigwa risasi na wengi wetu kufa. Haya yote ni kwa sababu ya kushinikiza mageuzi tunayotaka,” akasema Fadia Khalaf, ambaye ni mmoja wa waandamanaji.
Maafisa wa serikali wanasema karibu watu 65 wameuawa katika ghasia zinazohusiana na maandamano hayo tangu Desemba.
Awali, serikali ya Uganda ilikuwa imetangaza kujitolea kumpa hifadhi Bashir. “Ikiwa Bashir ataomba tumpe hifadhi humu, hilo ni suala ambalo linaweza kutathminiwa kwa urahisi na Rais Yoweri Museveni,” akasema Waziri wa Mashauri ya Kigeni nchini humo Okello Oryem.
Waziri huyo aliukosoa utawala wa kijeshi wa Sudan, akisema unapaswa kumheshimu kiongozi huyo kutokana na juhudi alizochukua katika kutafuta mwafaka wa amani nchini Sudan Kusini.?Rais Museveni amekuwa mojawapo wa washirika wa karibu wa Bw Bashir.
Baadhi ya nchi za Uarabuni kama Saudi Arabia na Milki ya Kiarabu (UAE) zimetangaza kuunga mkono utawala huo mpya wa kijeshi.