Kimataifa

Besigye ambaye bado anaishi jela, asusia kuanza kwa kesi akidai jaji anamwonea

Na REUTERS September 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KAMPALA, UGANDA

KIONGOZI wa upinzani Uganda Kizza Besigye amesusia kikao cha kuanza kwa kesi yake, akisema Jaji ambaye anasikiza kesi hiyo anamwonea na analenga kumhujumu.

Besigye amekuwa korokoroni kwa miezi kadhaa, hali ambayo imezua maswali iwapo Rais Yoweri Museveni kwa kweli anazingatia na kuheshimu haki za kibinadamu.

Museveni anasaka kuchaguliwa tena kwenye uchaguzi wa urais ambao utafanyika mnamo Januari mwaka ujao.

“Kusikizwa kwa kesi ya Besigye na msaidizi wake Obed Lutale kulistahili kuanza Jumatatu baada ya kucheleweshwa kwa miezi kadhaa.

Hata hivyo, wawili hao walisusia vikao vya kesi baada ya shinikizo za kumtaka Jaji Emmanuel Baguma ajiondoe kukosa kuzaa matunda.

Jaji Baguma mwenyewe alikataa kujiondoa katika kesi hiyo kwa mujibu wa wakili wa Besigye Eron Kiiza.

Wakili huyo alisema kuwa uamuzi wa Baguma kumnyima Besigye dhamana ndio umechangia wasusie vikao vya kesi.

“Hawezi kutoa uamuzi wa haki na wenye uwazi jinsi ambavyo inahitajika kwenye katiba. Besigye na Lutale wamesema hawatafika mbele ya jaji huyo,” akasema Wakili Kiiza.

Msemaji wa Mahakama James Mawanda alisema kuwa hakukuwa na haja ya kulaumiana na akadhibitisha kuwa Baguma alikuwa amekataa kujiondoa kwenye kesi ya Besigye.