Biden aendelea kumchoka kabisa Netanyahu kwa jinsi ‘anavyolipua raia’ Gaza
Na MASHIRIKA
WASHINGTON, Amerika
RAIS wa Amerika Joe Biden ameitaka Israel kulinda raia wa Palestina na wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada au Amerika ikome kuunga mkono Israeli katika vita vyake dhidi ya wapiganaji wa Hamas.
Kwenye ujumbe kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, Biden alikariri kuwa wanajeshi wa Israeli wanapaswa kukoma kuwashambulia “watu wasio na hatia” katika operesheni yao Ukanda wa Gaza.
Onyo la Amerika limejiri siku chache baada ya wafanyakazi saba wa shirika la kutoa misaada la World Central Kitchen (WCK) kuuawa, hatua iliyoibua kero kubwa ulimwenguni.
Israel inakubali kwamba ilikosea kwa kutekeleza shambulio la angani dhidi ya msafara wa wahudumu hao wa WCK.
Wadadisi wanabashiri kuwa endapo Bw Netanyahu atakaidi onyo hilo kutoka kwa Biden, huenda Amerika ikasitisha kutoa msaada wa silaha kwa Israel.
Aidha, itaondoa msimamo wake wa kuunga mkono Israeli katika Umoja wa Mataifa (UN).
“Hatua kama hii inakaribia kufika sawa na “kuwasili kwa Yesu”, akasema mdadisi Steven Cook mtaalamu katika Baraza kuhusu Mahusiano ya Kimataifa.
Alikuwa akirejelea kauli ya Biden mwezi jana kwamba yeye na Netanyahu wanaelekea hatua ya mwisho ya “kutofautiana”.
Dennis Ross, ambaye ni mwanadiplomasia wa Amerika anayehudumu katika taasisi ya ‘Washington Institute for Near East Policy’ akasema: “Kile Rais Biden anasema ni kwa Israel itimiza haya masharti ya kibinadamu la sivyo sitakuwa na jingine ila kukuwekea masharti kwa misaada ya kijeshi.”
Rais Biden, anayejitahidi achaguliwe tena katika uchaguzi wa Novemba, amekuwa akishinikizwa na wafuasi wa chama chake cha Democrats amchukulie Netanyahu hatua.
Wafuasi hao wa Democrat wamekerwa idadi kubwa ya raia wa Kipalestina wanaouawa na wanajeshi wa Israeli wakidai hatua hiyo itaathiri nafasi ya Biden kushinda urais.
Lakini hadi wakati huu, Rais Biden hajatoa masharti kuhusu msaada wa silaha kwa Israel.
Vita hivyo, vilianza baada ya wapiganaji wa Hamas kufanya msururu wa mashambulio kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7, 2023.
Watu 1,200 waliuawa kulingana na takwimu zilizotolewa na serikali ya Israel.
Mashambulio hayo ndio yalichangia Israeli kuanza kutekeleza mashambulio makali ya angani katika Ukanda wa Gaza wenye jumla ya watu 2.3.
Zaidi ya Wapalestina 33,000 wameuawa tangu wakati huo, kulinganana takwimu zilizotolewa na wizara ya Afya eneo hilo linalotawaliwa na Hamas.
Wengi wa waliouawa mni watoto, wanawake na wakongwe.
Israeli inaishutumu Hamas kwa kutumia raia kama ‘ngao’ ya kujikinga.
Ikulu ya White imesema kuwa sera ya Amerika kuhusiana na hali katika Gaza itegemea ukaguzi kuhusu iwapo Israel itatekeleza masharti yake kwamba ikomeshe mauaji ya raia.
Naye Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Amerika akasema hivi: “Angalia, nitasema hivi: ikiwa hatutaona mabadiliko tunayohitaji kuona, tutabadilisha sera yetu.”