• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 10:50 AM
Biden motoni wanaharakati Amerika wakitaka asiwanie urais

Biden motoni wanaharakati Amerika wakitaka asiwanie urais

NA MASHIRIKA

WASHINGTON, AMERIKA

WANAHARAKATI na watetezi wa haki za binadamu nchini Amerika sasa wanataka Rais wa nchi hiyo, Joe Biden, asiteuliwe kuwania kiti cha urais kwa msingi ya kuunga mkono Israeli katika mapigano yanayoendelea kati yake na Hamas.

Wanaharakati hao sasa wanataka kura ya mchujo wa mgombea urais wa Democrat utawaliwe na mada ya “sitisha mapigano”.

Wanadai kuwa Biden hafai kuteuliwa kuwania kiti hicho kulingana na jinsi anavyoshughulikia mzozo kati ya Israeli na Hamas.

Muungano huo wa wanaharakati wa kupinga vita vinavyoendelea ukanda wa Gaza, ulisema hatua hiyo itawapa nafasi wakazi wa nchi hiyo kupaza sauti zao dhidi ya Rais Biden kutokana na vifo vya raia katika Ukanda wa Gaza.

Wapigakura katika jimbo la Kaskazini Mashariki la New Hampshire walishiriki kura za mchujo jana na wito huo wa kuandika maneno “sitisha mapigano” kwenye karatasi za kura unalenga kuushinikiza utawala wa Biden.

Wanaharakati hao wameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X, kuwa utawala wa Biden kwa muda wa miezi mitatu iliyopita, umepuuza wito wa kutaka kusitishwa kwa vita na kukomesha uungaji mkono wao kwa Israeli.

Wakati huo huo, jimbo dogo la Kaskazini Mashariki mwa Amerika la New Hampshire jana lilifanya uchaguzi wa mchujo wa mgombea wa kiti cha urais.

Jina la Rais Biden halikujumuishwa kwenye kura hiyo ya mchujo.

Kathy Sullivan, ambaye ni mwenyekiti wa zamani wa chama cha Democratic katika Jimbo hilo alisema kwamba, “Watu walisema tutaliweka hilo pembeni na kwenda kumuunga mkono Joe Biden kwa sababu sote tunafahamu Donald Trump atakuwa mgombeaji na jambo muhimu tunaloweza kufanya ni kuokoa demokrasia kwa kumzuia Donald Trump.”

Haya yanajiri huku Biden na Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu, wakitofautiana hadharani kuhusu kitakachotokea Gaza mara tu vita vya Israeli na Hamas vitakapokamilika.

Biden na maafisa wake wakuu – akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken, ambaye alitembelea Israeli na eneo hilo wiki iliyopita – walisema kuundwa kwa taifa la Palestina lenye dhamana kwa usalama wa Israeli ndiyo njia pekee ya kuleta amani na utulivu katika Mashariki ya Kati.

Netanyahu kwa upande mwingine alisema wakati wa mkutano na wanahabari Alhamisi wiki jana kwamba alikataa wito huo akisema hatua kama hiyo itagongana na usalama wa Israeli.

“Katika mpango wowote ujao … Israeli inahitaji udhibiti wa usalama eneo lote la magharibi mwa Jordan. Hii inaenda kinyume na wazo la kuunda mamlaka (ya Palestina),” Netanyahu alisema.

  • Tags

You can share this post!

Wanaume watano wapatikana na hatia ya kuiba Sh15m kimabavu

Junet haendi popote, asema Raila

T L