Bobi Wine aachiliwa huru
MASHIRIKA na CHARLES WASONGA
MBUNGE wa upinzani na mwaniaji urais nchini Uganda, Robert Kyagulanyi, almaarufu Bobi Wine ameachiliwa huru saa kadha baada ya polisi kumkamata Jumatatu.
Mbunge huyo, ambaye pia ni msanii wa muziki, alikamatwa Jumatatu baada ya polisi kutibua mkutano aliopanga kuongoza katika eneobunge lake la Kyadondo Mashariki kuzindua kampeni zake za kuwania urais katika uchaguzi utakaofanyika mwaka 2021.
Alitarajia kutumia mkutano huo kutoa ufafanua kuhusu sera zake kabla ya kuanza rasmi kampeni zake za kumwondoa mamlakani Rais Yoweri Museveni ambaye ametawala nchi hiyo kwa zaidi ya miongo mitatu.
Hata hivyo Vuguvugu la Bobi Wine kwa jina People Power Movement limeahidi kuendelea na mikutano hiyo licha ya kuharamishwa na polisi.
Vilevile, maafisa wa polisi walidai kuwa mbunge huyo alipanga kuandaa mikutano haramu katika jiji kuu Kampala.
Maafisa wa serikali wanadai kuwa vuguvugu hilo halijatimiza sheria za kampeni na kanuni inayoongoza Mikutano ya Umma.
Kukamatwa kwa Bobi mnamo Jumatatu kulisababisha kero kote nchini Uganda huku kiongozi wa upinzani na aliyekuwa mwaniaji wa urais Dkt Kizza Besigye akiwashutumu maafisa wa polisi kwa hatua hiyo waliochukua dhidi ya Mbunge huyo.
Kwa mujibu wa Besigye, kukamatwa kwa Bobi Wine na kutawanywa kwa umati wa watu kwa vituo machozi katika miji ya Kasangati na Gayaza ni ukiukaji wa haki za kiraia