Kimataifa

Bobi Wine awekwa ‘chini ya kizuizi’ nyumbani

January 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MASHIRIKA

KAMPALA, UGANDA

KIONGOZI wa upinzani nchini Uganda, Robert Kyagulanyi, almaarufu Bobi Wine alisema jana amezuiliwa nyumbani kwake.

Bobi Wine, ambaye aliwania kiti cha urais alisema Alhamisi polisi walikuwa wamezingira makazi yake na kumweka “chini ya kizuizi cha nyumbani” kabla ya maandamano yaliyopangwa.

Wanasiasa wa upinzani walikuwa wamepanga maandamano siku ya Alhamisi kupinga hali mbaya ya barabara nchini Uganda, ambayo ni mwenyeji wa mikutano miwili ya kimataifa iliyoratibiwa kufanyika siku zijazo.

Bobi Wine, msanii aliyekuwa maarufu na kuingia katioka ulingo wa siasa, alisema polisi na wanajeshi wamemzuia kuondoka nyumbani kwake katika eneo la Magere, kaskazini mwa mji mkuu Kampala.

“Wanajeshieshi waoga na polisi wamezingira nyumba yetu na kutuweka chini ya kizuizi cha nyumbani, lakini maandamano yanaendelea,” kiongozi wa Jukwaa la Umoja wa Kitaifa (NUP) alisema kwenye mtandao wa X (awali Twitter).

“Rekebisha barabara zetu! Waachilie huru Wafungwa wa Kisiasa! Uganda Iwe huru!” akaandika.

Wine, alipingana na Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi uliopita wa Uganda mwaka 2021, akitaka utawala wa Rais Museveni aliodai ni wa kihimla ukomeshwe.

Aliyekuwa mgombea urais, Kizza Besigye wa chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change alisema Alhamisi kwamba yeye pia hakuruhusiwa kuondoka nyumbani kwake.

“Tumezuiliwa nyumbani na WAOGA! Hakuna kurudi nyuma; tunastahili bora zaidi. Tafadhali fanya uwezavyo, popote ulipo, kwa chochote ulicho nacho, ili kuonyesha barabara mbaya zinazokuathiri leo,” alichapisha kwenye X.

Msemaji wa polisi alithibitisha “maafisa wa polisi wanashika doria” nje ya makazi hayo mawili.

“Tumechukua baadhi ya hatua kuwazuia viongozi hao wawili kwani wanaweza kuwachochea baadhi ya watu kufanya mikutano isiyo halali na maandamano ya kisiasa,”, msemaji wa Polisi wa Jiji la Kampala, Bw Patrick Onyango aliiambia AFP.

“Kuna kikosi cha usalama katika nyumba za Bobi Wine na Dkt Besigye lakini sio kwa ajili ya kuwakamata lakini kama hatua ya kuzuia vurugu kulingana na majukumu ya polisi.”

Vyama vya upinzani vimeishutumu serikali kwa kuwaweka kizuizini watu wasio na makazi na kuharibu maelfu ya vibanda vilivyo kando ya barabara katika harakati za kufanya usafi kabla ya mikutano ya Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa na G77+China jijini Kampala.