Kimataifa

'Bora Uhai' ni msemo wa kiutumwa, afafanua Besigye

July 18th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa upinzani Uganda, Dkt Kizza Besigye, amesikitishwa vile watu hutumia msemo ‘Bora Uhai’.

Msemo huo ambao umepata umaarufu Kenya hasa miongoni mwa watumizi wa mitandao ya kijamii umekuwa ukitumiwa na watu kujieleza wakati wanapolemewa na jambo, na kuona ni afadhali wako hai.

Kulingana na Dkt Besigye, msemo huo ni miongoni mwa mengine ambayo yanadhihirisha wananchi hawana matumaini ya kuboreshewa hali yao ya kimaisha.

“Miaka mingi ya ukandamizaji imefanya sasa uwe ni jambo la kawaida unapozingatia baadhi ya misemo katika lugha zetu,” akasema, akitoa mfano wa ‘Bora Uhai’.

Akihutubu Jumatatu katika Hoteli ya Intercontinental, Nairobi, mwanasiasa huyo ambaye ni hasimu mkubwa wa miaka mingi wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, alisema raia wamenaswa kwenye minyororo ya utumwa na watu wachache wenye hadhi ya juu katika jamii na hivyo basi raia wanahisi hawajiwezi tena.

“Baada ya kupigania uhuru, watu wetu waliishiwa na nguvu za kubadilisha mambo nchini. Sasa tuna watu wa hadhi ya juu katika jamii ambao walirithi mamlaka ya ukandamizaji na raia hawana uwezo kabisa,” akasema.

Alitoa wito kwa mashirika ya kijamii kujitwika jukumu la kuhamasisha umma ili waelewe wako utumwani, na wachukue hatua zifaazo kujinasua.

“Raia anafaa kuwa mtu mwenye uwezo wa kubadilisha mambo. Jinsi ilivyo kwa sasa, sisi ni watumwa. Inafaa tujishughulishe na kubadilisha mawazo ya wananchi wtu. Wengi wao hawafahamu wametekwa utumwani,” akasema.

Hata hivyo, alionya dhidi ya utumiaji wa vita kutafuta mabadiliko na kusema mbinu hiyo huharibu hali zaidi kwani hugawanya taifa kwa muda mrefu.