Bosi aliyenaswa akimkumbatia mfanyakazi ajiuzulu
MKURUGENZI wa kampuni ya teknolojia, Astronomer, aliyenaswa akimkumbatia mfanyakazi mwenzake mwanamke kwenye tamasha ya bendi maarufu kama Coldplay kupitia video iliyosambazwa mno mitandaoni, amejiuzulu.
Katika taarifa Astronomer ilisema: “Andy Byron amejiuzulu na Bodi ya Wakurugenzi imekubali.”
Video hiyo ilionyesha mwanamume na mwanamke wakikumbatiana kwenye filamu kubwa katika ukumbi wa Foxborough, Massachusetts, kabla ya kuachiliana na kujitoa upesi kwenye kamera.
Wawili hao walitambulishwa na vyombo vya habari kuwa Byron, mkurugenzi wa Astronomer ambaye ameoa, na Kristin Cabot, Afisa anayesimamia waajiriwa.
Taarifa ya kampuni hiyo ilisema Jumamosi: “Jinsi tulivyoeleza awali, Astronomer inatilia maanani maadili na utamaduni ambao umetuongoza tangu ilipoanzishwa.”
“Viongozi wetu wanatarajiwa kudumisha viwango bora vya kinidhamu na uwajibikaji, na hivi majuzi, viwango hivyo havijatimizwa.”
Shirika hilo lililopo New York lilisema bodi itaanza kusaka kiongozi mpya na msimamizi wao wa bidhaa ataendelea kuhudumu kama kaimu mkurugenzi.
Video ya wawili hao wakifurahia mziki pamoja kwenye tamasha Jumatano usiku na kujaribu kujificha upesi ilitazamwa na mamilioni.
Baada ya kuwaona wawili hao wakikwepa, mwimbaji kiongozi wa Coldplay, Chris Martin, alieleza umati: “Ama wana mahusiano nje ya ndoa, au wana haya sana.”