Kimataifa

Buhari aahidi kuendelea kukabiliana na Boko Haram

May 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na AFP

ABUJA, Nigeria

RAIS wa Nigeria Muhamadu Buhari aliapishwa kuhudumu kipindi cha pili akiahidi kwa mara nyingine kupambana na changamoto za usalama na ufisadi katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Hata hivyo, maafisa walisema kando na gwaride la wanajeshi, sherehe hiyo iliyofanyika jijini Abuja ilikosa msisimko.

“Naapa kwamba nitakuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Nigeria. Na nitatetea na kulinda Katiba ya nchi,” Rais Buhari, 76,” akasema.

Makamu wa Rais Yemi Osinbaji pia aliapishwa.

Rais Buhari alichaguliwa tena katika uchaguzi uliofanyika Februari 2019 ambapo alipata asilimia 56 ya kura zilizopigwa.

Mpinzani wake mkuu Atiku Abubakar wa chama cha People Democratic Party (PDP) alikuwa wa pili kwa kupata asilimia 41 ya kura.

Hata hivyo, Bw Abubakar na viongozi wengine wa upinzani wamepinga ushindi wa Buhari kwa kuwasilisha kesi mahakamani. Wanadai uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu mkubwa.

Rais Buhari, ambaye zamani alikuwa kiongozi wa kijeshi, anaanza muhula wake wa pili huku taifa hilo likikabiliwa na changamoto nyingi, mojawapo ikiwa ni mashambulio ya kila mara yanayotekelezwa na wanamgambo wa Boko Haram kaskazini mwa Nigeria.

Kwa mfano, mnamo Jumanne usiku wapiganaji hao walishambulio mji wa Maiduguri ulioko Kaskazini Mashariki lakini wakazimwa na wanajeshi.

Imetafsiriwa na Charles Wasonga