Kimataifa

Bunge la Korea Kusini latishia kumtimua rais Yoon kwa kutangaza amri ya kijeshi

Na MASHIRIKA December 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WABUNGE wa Korea Kusini Jumatano walitisha kumtimua Rais Yoon Suk Yeol baada ya kutangaza sheria ya kijeshi na kuibatilisha saa chache baadaye, na kusababisha mzozo mkubwa zaidi wa kisiasa katika miongo kadhaa katika nchi yenye uchumi wa nne kwa ukubwa barani Asia.

Hatua hiyo iliyotangazwa siku ya Jumanne usiku iliwashangaza raia wa Korea Kusini, ambapo Yoon aliita jeshi ambalo lilitoa amri ya kupiga marufuku maandamano na shughuli za bunge na vyama vya kisiasa, na kuweka vyombo vya habari chini ya udhibiti wa serikali.

Lakini wabunge 190 kati ya 300 wa Bunge la Kitaifa walikaidi  polisi na jeshi na wakapiga kura kukataa tangazo hilo, ambalo Yoon alilazimika kuliondoa chini ya saa mbili baada ya kulitamka.

Yoon alisema vyama vya upinzani vimeteka mchakato wa bunge.

“Ninatangaza sheria ya kijeshi ili kulinda Jamhuri ya Korea huru dhidi ya tishio la vikosi vya Kikomunisti vya Korea Kaskazini, kutokomeza vikosi vya serikali ya Korea Kaskazini ambavyo vinapora uhuru na furaha ya watu wetu, na kulinda uhuru wa kikatiba,” Yoon alisema.

Yoon hakutaja tishio lolote maalum kutoka Korea Kaskazini nchi iliyo na silaha za nyuklia, badala yake alilenga wapinzani wake wa kisiasa wa ndani.

Hoja zilizowasilishwa

Alilalamikia hoja 22 zilizowasilishwa kutimua maafisa wa utawala wake tangu aingie madarakani Mei 2022.

Umaarufu wa rais huyo umeshuka kwa kiwango kikubwa huku kukiwa na kashfa  na migongano na bunge linalodhibitiwa na upinzani kuhusu bajeti na uchunguzi.

Jeshi lilimtaja Mkuu wa Jeshi Jenerali Park An-su, kiongozi wa kamati ya sheria ya kijeshi kuanzia saa tano  Jumanne usiku.

Kando na kupiga marufuku shughuli za kisiasa na kuzuia vyombo vya habari, amri hiyo pia iliamuru madaktari wanaogoma kurejea kazini na wale ambao wangekiuka wangekamatwa.

Wanajeshi waliofunika nyuso wakiwa na bunduki, na vifaa vya kuona usiku waliingia Bungeni ambako walikabiliana na wafanyakazi waliowapiga kwa vifaa vya kuzimia moto.

Maelfu ya waandamanaji walikusanyika nje ya bunge ambapo kulikuwa na makabiliano madogo na polisi na wanajeshi.

Wabunge walikusanyika kupiga kura dhidi ya sheria ya kijeshi, huku wabunge wa upinzani na viongozi wa chama cha Yoon wakitaja amri hiyo kinyume cha katiba.

Kura ya kuondoa sheria

Wabunge wote 190 waliokuwepo walipiga kura kuondoa sheria ya kijeshi, wakiwemo 18 kutoka chama cha Yoon mwenyewe.

Yoon aliamuru wanajeshi kurudi kambini na baadaye akaondoa amri hiyo baada ya kuitisha mkutano wa baraza la mawaziri.

Baadhi ya balozi za kigeni mjini Seoul zilionya raia wao kuchukua tahadhari.

Maafisa wa Amerika, Uingereza, Ujerumani, na nchi nyingine walisema wana wasiwasi kuhusu matukio hayo na kusema utawala wa amani wa sheria unapaswa kutawala.

Wabunge wa upinzani walimtaka Yoon ajiuzulu la sivyo aondolewe mamlakani. Mkuu wake wa majeshi na maafisa wengine walijitolea kujiuzulu kwa wingi, huku kiongozi wa chama tawala akitaka waziri wa ulinzi afutwe kazi na baraza zima la mawaziri kujiuzulu.

Maandamano zaidi yanatarajiwa huku muungano mkubwa wa vyama vya wafanyakazi nchini Korea Kusini, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini Korea, ukipanga kufanya maandamano mjini Seoul na kuapa kugoma hadi Yoon ajiuzulu.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA