Kimataifa

Chakwera hatarini kuwa ‘Wantam’ baada ya mtangulizi wake kuweka kampeni kali Malawi

Na MASHIRIKA September 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

LILONGWE, MALAWI

RAIS Lazarus Chakwera amejikuta kwenye kinyang’anyiro kikali cha kusalia mamlakani dhidi ya mtangulizi wake Peter Mutharika, katika uchaguzi unaotishia kumfanya ‘Wantam’.

Joto la kisiasa linaendelea kupanda Malawi huku kampeni zikiingia mkondo wa lala salama kuelekea uchaguzi mkuu utakaoandaliwa Jumanne ijayo.

Kura hiyo inawaniwa na wagombeaji 17 lakini kibarua kikali kipo kati ya Rais Chakwera, 70 na rais wa zamani Mutharika, 84.

Chakwera ndiye kiongozi wa MCP na anasaka uungwaji mkono kuingia muhula wa pili.

Kwa upande mwingine, Mutharika anawania kupitia DPP.

Chakwera alimshinda Mutharika katika uchaguzi mkuu wa 2020 ambao ulirudiwa baada ya Mutharika kumshinda katika mkondo wa kwanza lakini akakosa kupata asilimia 50 za kura jinsi katiba ya nchi hiyo inavyosema.

Pia kinyanga’nyironi kuna Joyce Banda, 74, ambaye alikuwa rais kati ya 2012-2014.

Utawala wa Chakwera ambaye alikuwa mhadhiri wa somo la Dini, umekuwa ukiandamwa na changamoto tele za kiuchumi huku akikumbwa na madai mengi ya ufisadi.

Kwa upande mwingine, anasifiwa kwa kurejesha huduma za treni Malawi kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30.

Pia utawala wake unasifika kwa ujenzi wa barabara kuu katika taifa hilo.

Mutharika ambaye alikuwa wakili na mhadhiri naye anaponzwa na umri japo alikuwa Rais wa Malawi kati ya 2014-2020.

Ni nduguye Bingu wa Mutharika ambaye aliaga dunia akiwa afisini mnamo 2012.

Sawa tu na Chakwera, Mutharika pia anaandamwa na madai ya ufisadi na wakati wake uchumi wa taifa pia ulikuwa mbaya.

Hata hivyo, wandani wake wanasema kuwa hali ilikuwa afadhali alipokuwa madarakani na alisimamia vyema nchi na sarafu za nchi hiyo zilikuwa na thamani kubwa.

Umri mkubwa wa Mutharika pia umechangiwa na hofu kuhusu siri inayogubika hali yake ya kiafya.