China yaonya Ufaransa dhidi ya kutetea Hong Kong
NA MASHIRIKA
RAIS wa Ufaransa, Emmanuel Macron Jumatatu alianza ziara rasmi nchini Uchina huku wenyeji wakimuonya dhidi ya kuzungumzia maandamano ya kupigania demokrasia yanayoendelea Hong Kong.
Macron anatarajiwa kuhudhuria Kongamano la Kimataifa la Kibiashara jijini Shanghai na anatarajiwa kuandaa mazungumzo na Rais Xi Jinping kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu mataifa hayo mawili.
Raia wa Hong Kong wamekuwa wakiandamana kupigania uhuru wao wa kidemokrasia baada ya sheria na sera nyingi za utawala wa Uchina kutumika katika mji huo ambao wakazi wake wanadai utawala wake haufai kushirikisha Beijing.
Vilevile kumekuwa na malalamishi mengi kuhusu hatua ya serikali ya Uchina kuwazuilia Waislamu wengi katika eneo la Xinjiang, Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo.
“Hong Kong na Xinjiang ni masuala ya ndani ambayo yanatatuliwa na Uchina. Si vyema kuyaweka kama ajenda ya kujadiliwa kati ya viongozi hao wawili,” akasema Zhu Jing wa Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Uchina.