Kimataifa

China yashika Trump pabaya, ubabe wa kibiashara ukiendelea

Na REUTERS February 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BEIJING, CHINA

UHASAMA wa kibiashara kati ya Amerika na China ulizidi Jumanne baada ya China nao kuweka ushuru wa juu kwa bidhaa za Amerika ambazo zinaingizwa nchini humo.

Ubabe wa kibiashara kati ya nchi hizo zenye uchumi mkubwa duniani umechipuka wakati ambapo Rais Donald Trump anaendelea kutekeleza mabadiliko ya kisera na kiuchumi dhidi ya washirika wa kibiashara wa Amerika.

Baada ya kuwekea Mexico na Canada vikwazo vya kiuchumi, kiongozi huyo Jumanne aliviondoa ili kupisha mazungumzo.

Vikwazo vyake vilikuwa vikilenga kupunguza idadi ya wahamiaji haramu wanaoingia Amerika kutoka mataifa hayo mawili.

Amerika Jumatatu iliongeza ushuru kwa asilimia 10 kwenye bidhaa za China. Hii ni baada ya Rais Trump kutoa onyo kuwa Beijing haikuwa ikifanya jambo lolote la maana kuzuia dawa za haramu kuingia Amerika.

China nayo ilijibu kupitia wizara yake ya kifedha, ikisema kuwa itaongeza ushuru wa asilimia 15 kwa bidhaa za Amerika kama mafuta ghafi, pembejeo za kilimo, vipuri vya magari na makaa ya mawe.

Pia China ilitangaza kuwa inalenga kuharamisha kampuni za Google, Calvin Klein na ile ya kiteknolojia ya Illumina kwenye orodha ya kampuni za Amerika ambazo zimekubali kufanya biashara nchini humo.

Kama hayo hayatoshi, China inalenga kudhibiti vifaa vya kielektroniki na kawi safi ambazo imekuwa ikiuzia Amerika. China ilisema vikwazo na nyongeza ya ushuru kwa Amerika itaanza kutekelezwa rasmi mnamo Februari 10.

Mwanya huo wa siku tano unalenga kuhakikisha kuwa nchi hizo mbili zinaafikiana kuhusu utata wa kibiashara uliochipuka. Rais Trump amepangiwa kuzungumza na mwenzake wa China Xi Jinping baadaye wiki hii kwa mujibu wa taarifa zilizotoka Ikulu ya White House.

Trump hasa ameonya kuwa ataongeza ushuru zaidi kwenye bidhaa za China hadi pale nchi hiyo izime kabisa kuingizwa kwa dawa hatari ya fentanyl. Dawa hiyo hutumika kupunguza maumivu kwa wagonjwa hasa wale wa kansa.

“Wasipokoma kutuma dawa hiyo hatari Amerika, ushuru huu utapanda zaidi,” akasema mnamo Jumatatu.

Ingawa hivyo, China imesema tatizo la fentanyl ni la Amerika na imeapa kupinga vikwazo na nyongeza ya ushuru kutoka kwa Amerika kwenye Shirika la Kibiashara Ulimwenguni (WTO).

China haitegemei Amerika sana kwa mafuta ghafi na mwaka jana ilitumia mafuta ya thamani ya Sh775 bilioni. Pia ni asilimia tano tu ya gesi ambayo China hutumia hutoka Amerika.

Wachanganuzi wa masuala ya kiuchumi wamebashiri kuwa itakuwa vigumu kwa China kuridhia matakwa ya kisiasa na kiuchumi kutoka kwa Rais Trump. Wanasema kuwa huenda Amerika ikatumia suala la kuongeza ushuru na vikwazo vya kiuchumi kudhidhirisha ubabe wao.

Mnamo Jumapili, Rais Trump alisema sasa analenga Umoja wa Bara Ulaya (EU) kwa kuiwekea vikwazo vya kibiashara. EU ndiyo mshirika mkubwa wa kibiashara wa Amerika.

Hata hivyo, vikwazo hivyo vitaisaza Uingereza ambayo ilitoka EU mnamo 2020.