Kimataifa

China yatenga watu 30 milioni miji 10 kutokana na virusi

January 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na AFP

CHINA imeongeza miji iliyotengwa katika juhudi za kukabiliana na virusi vya homa kali ya COV, iliyoua watu 26 kufikia sasa hatua ambayo imeathiri zaidi ya watu 30 milioni.

Hatua hiyo ilijiri huku Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) likichelea kutangaza virusi hivyo hatari kuwa janga la kimataifa likisema China imechukua hatua za kuvidhibiti.

Sherehe za mwaka mpya maarufu kama Lunar nchini humo zilifutwa na maeneo ya burudani ya Forbidden City mkoani Beijing na Disneyland katika mkoa wa Shanghai yakifungwa kuzuia kuenea kwa maradhi hayo.

Virusi hivyo ambavyo havikuwa vikijulikana vimezua wasiwasi kwa sababu vinafanana na vile vya SARS vilivyoua watu wengi China na Hong Kong miaka ya 2002 na 2003.

WHO ilisema China inakabiliwa na janga la kitaifa lakini ikakataa kutangaza kuwa suala la dharura hatua ambayo ingefanya jamii ya kimataifa kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuiwekea vikwazo vya usafiri na biashara.

Virusi hivyo vilizuka katikati ya likizo ya Lunar New Year inayosherehekewa kwa mikutano ya familia na umma.

Maradhi hayo yaligunduliwa kwa mara ya kwanza Desemba katika mji wa Wuhan ulio na watu 11 milioni na yameenea hadi nchi nyingine ikiwemo Amerika.

Mnamo Ijumaa, jiji la Wuhan barabara zilikuwa zimehamwa na duka kufungwa.

Hata hivyo, hospitali ambazo wanahabari wa AFP walitembelea zilikuwa zimejaa wagonjwa waliokuwa wakikaguliwa na maafisa waliovalia mavazi ya kuwakinga.

Mbali na Wuhan, miji mingine minane pia ilitengwa na hatua za tahadhari kuchukuliwa.

Mji wa hivi majuzi kufungwa ni Jingzhou, ulio na watu zaidi ya milioni tano ambao ulifungwa Ijumaa kwa kusitisha shughuli zote za uchukuzi wa umma.

Jijini Wuhan, maafisa wa serikali walipunguza idadi ya teksi kuanzia Ijumaa na kampuni kubwa ya teksi ya Didi Chuxing ikatangaza kuwa itasimamisha huduma jijini humo.

Hafla zote za umma zimefutwa Beijing na mnamo Ijumaa, maafisa waliovalia mavazi ya kuwakinga walikuwa wakipima kiwango cha joto watu wote waliokuwa wakiingia.

Maafisa wa serikali walisema idadi ya watu walioambukizwa ni zaidi ya 800 huku 177 wakiwa mahtuti. Maafisa wa afya walikuwa wakichunguza watu 1,072 walioshukiwa kupata virusi hivyo.

China imepongezwa kwa hatua ilizochukua tofauti na ilivyokuwa wakati virusi vya SARS vilipozuka ilipozuia wataalamu wa WHO.