Kimataifa

Corona inaongeza pengo kielimu kati ya watu maskini na matajiri

September 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

PARIS, Ufaransa

PENGO la usawa wa kielimu kati ya watu maskini na matajiri litaongezeka sana kwa sababu ya hatua ya serikali mbalimbali ulimwenguni kufunga shule kwa hofu ya janga la corona, ripoti imeonyesha.

Ripoti hiyo ilitolewa na Shirika la Ushirikiano kuhusu Uchumi na Maendeleo ambalo lilifanya utafiti katika mataifa mbalimbali.

Serikali katika mataifa mengi kote duniani zilifunga shule ili kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona, kwa muda wa karibu wiki 10 au zaidi ya nusu ya mwaka wa shule.

Athari mojawapo iliyojitokeza ni kuwa watoto walio na intaneti, tarakilishi na familia zilizowasaidia, walikuwa na wakati rahisi kuendelea na elimu.

“Wanafunzi kutoka familia tajiri wanaweza kujiendeleza licha ya shule kufungwa, kupitia tasnia mbadala za elimu. Wale wa kutoka familia maskini aghalabu walibaki wakiwa wamefungiwa nje shule zilipofungwa,” ilisema ripoti hiyo.

Athari nyingine ya kufunga shule ni kuwa itasababisha kupotea kwa ujuzi hali ambayo huenda ikasababisha uzalishaji kiuchumi duniani kushuka kwa asilimia 1.5 katika muda uliosalia kwenye karne hii.

“Kukosekana kwa elimu kutasababisha ujuzi kutoweka na ujuzi ulio na watu unachangia uzalishaji wao,” ilisema ripoti hiyo, ikifafanua utabiri kuhusu kushuka kwa GDP ulimwenguni.

Huku shule katika mataifa mengi zikifunguliwa tena, bado kuna changamoto kuu kwa sekta ya elimu, kulingana na ripoti ya OECD.

Ni sharti shule zitafute namna ya kufungua tena bila kusababisha kuongezeka kwa maambukizi mapya.

Kulingana na ripoti hiyo, huku mifumo ya kiuchumi ikiporomoka, kuna tishio kwamba bajeti za elimu zitapungua na vyuo vikuu vitahitajika kujiimarisha upya kivyao. ili viweze kuendelea kuvutia wanafunzi hata wakati havitaweza tena kutoa mafunzo ya kawaida.

Janga hilo hasa limeathiri zaidi mafunzo ya kiufundi, hali ambayo imeibua wasiwasi mkuu, kwa sababu wataalam wengi waliokuwa kiungo kikuu kiuchumi na kijamii wanategemea kufuzu kimasomo.

“Serikali zinapaswa kuzidisha juhudi za kufanya mafunzo ya kielimu na kiufundi kuwa ya kuvutia zaidi kwa vijana. Haya yanapaswa kujumuisha mafunzo kazini na kuimarisha mahusiano na sekta ya kibinafsi,” ilisema ripoti.

Hata hivyo, ripoti hiyo inasema ni rahisi zaidi kwa wanafunzi kusonga kutoka masomo ya kiufundi hadi elimu ya juu ambayo pia ni muhimu na yanaweza pia kuboresha matokeo ya masomo.

Aidha, ripoti hiyo ilisema kuwa janga hilo limeibua wasiwasi kote ulimwenguni kuhusu thamani ya taasisi za elimu ya juu, huku wanafunzi wakichelea kuwekeza kiasi kikubwa cha muda na hela wakati kiasi kikubwa cha kazi kinapatikana mitandaoni.