• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 11:30 AM
CORONA: Kenya yafuta kuwa mwenyeji mikutano na makongamano ya kimataifa

CORONA: Kenya yafuta kuwa mwenyeji mikutano na makongamano ya kimataifa

Na MARY WANGARI

NAIROBI, KENYA

RAIA wa kigeni waliokuwa wamepanga kuhudhuria makongamano ya kimataifa nchini Kenya watalazimika kufutilia mbali ziara zao kwa sababu serikali imepiga marufuku mikutano yote ya kimataifa kwa kipindi cha mwezi mmoja ujao.

Hatua hii imejiri huku taharuki ikizidi kutanda kuhusu tishio la mkurupuko wa virusi vya Corona nchini ambapo Afrika Kusini ilithibitisha kisa cha kwanza cha maambukizi ya ugonjwa huo mnamo Alhamisi.

Akizungumza Ijumaa katika uzinduzi wa kitengo cha wagonjwa waliotengwa katika Hospitali ya Mbagathi, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe ametangaza kuwa mikutano na makongamano yote yanayohusisha raia wa kigeni zaidi ya 15 sasa ni marufuku nchini.

“Serikali imepiga marufuku mara moja mikutano na makongamano yote ya hadhi ya kimataifa nchini Kenya. Ikiwa kongamano linahusu zaidi ya watu 15 wanaosafiri kutoka mataifa mengine duniani, serikali imeagiza mikutano hiyo isitishwe kwa kipindi cha siku 30 zijazo,” amesema.

Aidha, amesema kwamba serikali imewatahadharisha Wakenya dhidi ya kusafiri katika mataifa yanayoathiriwa na mkurupuko huo.

“Serikali pia imetoa ilani ya usafiri kwa Wakenya wote kujiepusha na safari zisizo muhimu katika mataifa hatari kuhudhuria mikutano ya zaidi ya watu 15,” alisema.

Hata hivyo, Bw Kagwe alifafanua kwamba mikutano yote ya Wakenya isiyohusisha raia wa kigeni itaendelea kama kawaida.

Kulingana naye, Mbio za Beyond Zero zinazoongozwa na Mama Taifa Margaret Kenyatta, mkewe Rais Uhuru Kenyatta, ambazo zimepangiwa kufanyika Jumapili zitaendelea jinsi ilivyopangwa.

Michuano ya Kenya Open iliyopangiwa kufanyika kuanzia Machi 12 -15 katika Karen Country Club ni mojawapo ya hafla za kimataifa zitakazoathirika kutokana na marufuku hiyo.

Isitoshe, serikali imetoa kibali cha muda kwa shirika la ndege la Italia kuingia nchini kuwachukua raia wake waliokwama.

“Tumesimamisha kwa muda marufuku kwa safari moja tu ya ndege kutoka Italia ili ije Kenya kuchukua watu waliokwama tulipokomesha safari kutoka Verona, Milan na Italia Kaskazini. Kuna watu wapatao 800 waliofungiwa Malindi, Tumeruhusu ndege tupu kuja bila abiria yeyote, Hakuna atakayeshuka ndege hiyo, ni wale tu abiria watakaoabiri,” amesema

Bw Kagwe ameeleza kwamba Wizara ya Uchukuzi vilevile imeandaa kikao na wamiliki wa vyama vya matatu na bodaboda kwa lengo la kuwahamasisha kuhusu usalama wa abiria.

Huku akiwaonya wanaoeneza ripoti za uongo kwamba watashtakiwa, waziri ameeleza kwamba serikali kwa ushirikiano na kampuni ya mawasiliano ya Safaricom itakuwa ikiwatumia jumbe wananchi katika juhudi za kuwahamasisha kuhusu virusi vya Corona na jinsi ya kujikinga.

“Wakenya wanapaswa kuwa makini kwa kuwa tishio bado ni kuu huku tukiendelea kuzingatia mikakati ya kujikinga. Zingatia usafi wa kimsingi na hali ya hewa. Tutakuwa tukiwatumia jumbe watu binafsi kuhusu jinsi ya kujikinga,” amesema.

You can share this post!

Chebukati atoa ufafanuzi kumhusu Igathe

TAHARIRI: Mara hii Chui ana kucha dhidi ya Gor

adminleo