Kimataifa

Corona yavamia Wabunge 23, yazua wasiwasi mkuu

March 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

TEHRAN, IRAN

HOMA ya Corona imevamia bunge la Iran huku wabunge 23 wakithibitishwa kuwa na maradhi hayo hatari ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 3,203 kote duniani.

Jumla ya watu 2,300 wameambukizwa virusi vya Corona nchini Iran na watu 77 wamethibitishwa kufariki.

Iran ndio nchi iliyoathiriwa zaidi na virusi nje ya China ambayo imepoteza zaidi na watu 3,000 kutokana na maradhi hayo.

Jumla ya maafisa 300,000, wakiwemo wahudumu wa afya na wanajeshi, wametumwa katika vituo mbalimbali vya afya katika juhudi za kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Shirika la habari la Fars News liliripoti kuwa waathiriwa 435 waliokuwa na homa ya Corona walitibiwa na kupona.

Serikali ya Iran Jumanne alisema kuwa wabunge 23 ambao ni sawa na asilimia 8 ya wabunge wa nchi hiyo, wameathiriwa na virusi vya Corona.

Jumatatu, mshauri wa Kiongozi wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei alifariki kutokana na virusi vya Corona.

Naibu wa Rais pamoja na naibu waziri wa afya pia wanaendelea kutibiwa hospitalini baada ya kupatikana na virusi vya Corona.

Kiongozi wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei Jumanne aliagiza wanajeshi kuingilia kati katika kuzuia kusambaa kwa maradhi hayo lakini hakuelezea ni mbinu ipi wanajeshi hao watatumia kuzuia kusambaa kwa homa hiyo.

“Ugonjwa huu si wa kushtua sana, tumewahi kushuhudia majanga makubwa kuliko homa ya Corona. Si kwamba nadharau Corona ila sitaki watu wadhani kuwa ugonjwa huo utatumaliza,” akasema Khamenei, kulingana na shirika la habari la Mehr la nchini Iran.

Serikali ya Iran ilikataa hatua ya wataalamu kutoka Amerika kuja kuwasaidia kukabiliana na maambukizi ya homa ya Corona.

Wiki iliyopita, Waziri wa Mashauri ya Mataifa ya Kigeni wa Amerika Mike Pompeo alidai kuwa serikali ya Iran inajaribu kuficha idadi halisi ya watu walioathiriwa na hata kufariki kutokana na maradhi ya Corona. Watu zaidi ya 92,000 wameambukizwa homa ya Corona kote duniani na kati yao, asilimia 3.2 wamefariki.

Mbali na China na Iran, mataifa mengine ambayo yameripoti visa vingi vya waathiriwa wa Corona ni Italia (2,502), Korea Kusini (5,186), Ufaransa (212), Japan (705), Malaysia (36), Uswizi (23), Norway (32), Singapore (110), Uhispania (149), Amerika (106) na Uingereza (51).

Waziri wa Afya wa India alitangaza Jumatano kuwa raia 14 kati ya 21 wa Italia waliozuru nchi hiyo walipatikana na virusi vya Corona.

Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in amefutilia mbali ziara yake katika Miliki za Uarabuni (UAE), Misiri na Uturuki kutokana na hofu ya homa ya Corona.