Coronavirus sasa yaua watu 2004
NA MASHIRIKA
IDADI ya watu waliofariki kutokana na homa ya Corona (Covid-19) imefikia 2004, kulingana na Tume ya Kitaifa ya Afya ya China.
Jumla ya watu 132 walifariki kati ya Jumapili na jana katika mkoa wa Hubei ambao umeathiriwa zaidi na maambukizi ya virusi hivyo.
Tume hiyo ilisema kuwa jumla ya watu 74,185 wameambukizwa virusi hivyo nchini China.
Hayo yanajiri huku Urusi ikitangaza kuwa itazuia raia wa China kuingia nchini humo kuanzia leo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres jana alisema kuwa homa ya Covid-19 “imefikia hali ya hatari sana na ni vigumu kuzuia maambukizi yake”.
Wakati huohuo, serikali ya China jana ilifutilia mbali vibali vya wanahabari watatu wa gazeti la Wall Street Journal la nchini Amerika kwa kuchapisha kichwa cha habari kilichorejelea taifa hilo la Asia kama “nchi yenye ugonjwa”.
Msemaji wa serikali ya China, Geng Shuang jana alisema kuwa gazeti la Wall Street Journal lilidunisha nchi hiyo na kuibagua kwa misingi ya rangi.
Geng Shuang alisema kuwa gazeti hilo limekataa kuomba msamaha wala halijawachukulia hatua wahariri walioandika tahariri hiyo.
Hayo yanajiri huku wanafunzi kutoka Pakistan wanaosomea nchini China wakilalama kuwa wametelekezwa na serikali ya nchi yao.
Wanafunzi hao wanasema kuwa juhudi zao za kuifikia serikali ya Pakistan kuwaokoa kutoka maeneo yaliyoathiriwa na homa ya Covid-19 nchini China zimeambulia patupu.
“Serikali ya Rais Imran Khan imetutelekeza na kufikia sasa hakuna mtu ambaye amewasiliana nasi,” wakasema wanafunzi hao.
Korea Kusini jana ilitangaza kuwa idadi ya watu ambao wameambukizwa virusi vya Covid-19 imeongezeka kutoka 31 hadi 51.
Taasisi ya Kutafiti Maradhi ya Korea Kusini (KCDC) ilisema kuwa visa vipya 20 vya waathiriwa wa homa ya Covid-19 viliripotiwa ndani ya wiki moja iliyopita.
Chama tawala nchini China kimetishia kuadhibu viongozi wa eneo la Wuhan ambapo mkurupuko wa homa ya Covid-19 ulianzia, iwapo watashindwa kuzuia maambukizi zaidi ya virusi hivyo hatari.
Chama hicho kiliagiza maafisa wa serikali na wahudumu wa afya kuhakikisha kuwa wakazi wote wa jiji la Wuhan walioathiriwa na virusi hivyo wanatengwa.
Jumatano, viongozi wa serikali na wahudumu wa afya walikuwa wakitembea kutoka nyumba moja hadi nyingine wakigawa kofia na mavazi ya kukinga watu dhidi ya kupatwa na virusi hivyo.
“Maisha ya binadamu ni muhimu. Ikiwa kisa chochote cha maambukizi mapya ya homa hiyo kitapatikana baada ya Alhamisi (leo), maafisa wa serikali wa eneo hili wajiandae kadhibiwa,” akasema Wang Zhonglin, Katibu Mkuu mpya wa chama tawala cha Communist.