COVID-19: WHO yaelezea matumaini ya kupatikana chanjo mwishoni mwa 2020
CHARLES WASONGA na MASHIRIKA
CHANJO dhidi ya Covid-19 itakuwa tayari ikifikapo mwishoni mwa mwaka huu 2020, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema Jumanne, bila kutoa ufafanuzi.
Kwa hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Tedros Adhanom Ghebreyesus aliwataka viongozi wote wa mataifa ya ulimwengu kushirikiana kuhakikisha kuwa chanjo hizo zinapatikana kwa usawa.
“Tutahitaji chanjo na kuna matumaini kwamba ifikapo mwisho wa mwaka huu tunaweza kupata chanjo mufti za kudhibiti virusi vya corona,” Tedros akasema katika hotuba ya kufunga mkutano wa bodi ya WHO iliyokuwa ikijadili mikakati ya kupambana na janga hili.
Mkutano huo ulifanyika jijini Geneva, Uswisi.
Chanjo tisa zimeorodheshwa na WHO kwa ajili ya kufanyiwa majaribio.
Majaribio hayo yanaongozwa na taasisi kwa jina COVAX inayomilikiwa na shirika hilo la afya ulimwenguni na ambayo inalenga kusambaza vipimo 2 bilioni vya chanjo hizo ifikapo mwishoni mwa mwaka wa 2021.
Kufikia sasa mataifa 168 yamejiunga katika mpango huo unaoendeshwa na taasisi ya COVAX.
Hata hivyo, mataifa ya China, Amerika na Urusi sio miongoni mwa mataifa hayo.
Rais wa Amerika Donald Trump amesema badala yake, serikali inategemea ushirikiano kati yake na mataifa kadhaa ili kupata chanjo hizo kutoka kwa kampuni za kuzitengeneza.
Kiongozi huyo ambaye juzi alipatikana na virusi vya corona, anaendelea kupata afueni huku akiendelea kupokea matibabu.