Kimataifa

Dawa aina mbili zaonyesha mafanikio makubwa kukabili Ebola

August 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na AFP na MARY WANGARI

WANASAYANSI wamesema wanakaribia kupata tiba ya kwanza mwafaka dhidi ya virusi vya Ebola baada ya aina mbili za dawa kuonyesha mafanikio ya hadi asilimia 90 ya kunusuru wagonjwa zilipofanyiwa majaribio katika kliniki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Aina hizo mbili za dawa zilizokuwa zikifanyiwa majaribio – Regeneron’s REGN-EB3 na nyingine ya kuimarisha kinga mwilini, mAb114 – zilitengenezwa kwa kutumia seli za kupigana na maradhi mwilini zilizokusanywa kutoka kwa manusura wa maambukizi ya Ebola.

Dawa hizo zilionyesha matokeo bora zaidi miongoni mwa wagonjwa katika majaribio ya tiba nne yanayofanywa tangu kutokea kwa mkurupuko wa pili mkubwa zaidi wa Ebola kutokea katika historia, ambao sasa unaingia mwaka wake wa pili nchini DRC.

“Kuanzia sasa, hizi ndizo dawa pekee zitakazotumika kuwatibu wagonjwa katika siku za usoni, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema katika taarifa iliyotolewa mnamo Jumatatu.

Dawa hizo ziliimarisha zaidi uwezo wa kunusurika kutokana na maradhi hayo kushinda aina nyingine mbili za tiba zinazofanyiwa majaribio – ZMapp, iliyotengenezwa na Mapp Biopharmaceutical, na Remdesivir, iliyotengenezwa na Gilead Sciences.

Majaribio hayo yaliyoanza mnamo Novemba 2018 yanafanywa na kundi la kimataifa la utafiti linaloelekezwa na WHO.

Bw Anthony Fauci, mmoja wa watafiti wanaoongoza shughuli hiyo ya majaribio, na mkurugenzi wa Taasisi ya Kitaifa Amerika kuhusu Mzio na Maradhi ya Maambukizi, alieleza wanahabari kwamba matokeo hayo yalikuwa “habari njema sana” kwa vita dhidi ya Ebola.

“Inamaanisha kwamba sasa tuna kile kinachoonekana kama tiba (mbili) dhidi ya ugonjwa ambao majuzi tu hatukuwa na mwelekeo wowote wa kuukabili.”

Ebola imekuwa ikisambaa Mashariki mwa DRC tangu Agosti 2018 katika mkurupuko ambao sasa umegeuka wa pili mkubwa zaidi, uliowaua watu wasiopungua 800.

Juhudi za kuudhibiti zimelemazwa na michafuko ya kivita, huku wahudumu wa kukabiliana na dharura wakihangaika kupata ushirikiano wa jamii zilizoathiriwa, wengi wao wakiwa hawana imani na serikali na uzinduzi wa mikakati ya kimatibabu – inayosimamiwa na vikosi vya usalama – inayokinzana na itikadi za wanajamii eneo hilo.

Mkurupuko wa Ebola eneo la Afrika Magharibi uligeuka mkubwa zaidi kutokea ulimwenguni uliposambaa kupitia Guinea, Liberia na Sierra Leone kutoka 2013 hadi 2016 na kuwaua watu zaidi ya 11 300.

Mike Ryan, anayeongoza mradi wa WHO wa kukabiliana na majanga ya dharura alisema matokeo hayo mema yalikuwa ya kutia moyo lakini hayajitoshelezi kuangamiza kabisa Ebola.

Tayari WHO imewashauri wagonjwa wa Ebola kutafuta dawa hizo zilizoonyesha mafanikio.