EU yaifaa Kenya Sh7.8 bilioni ipambane vilivyo na janga la Covid-19
Na CHARLES WASONGA
NAIROBI, Kenya
UMOJA wa Ulaya (EU) umeipa Kenya msaada wa takriban Sh7.8 bilioni kufadhili mipango ya kukabiliana na makali ya janga la Covid-19.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, EU imesema pesa hizo zinalenga kusadia Wakenya wanaokabiliwa na hatari ya kusakamwa na njaa kando na kufadhili mipango ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.
Msaada huo unajumuisha Sh3.6 bilioni za kupiga jeki bajeti ya Serikali ya Kenya ya ununuzi wa vifaa vya kuzuia maambukizi na athari za Covid-19 katika sekta za afya, kijamii na kiuchumi.
Sh1.2 bilioni zimetengewa mipango ya kuzisaidia familia zilizoathirika na makali haya na ambazo zinaishi katika mitaa ya mabanda.
Pesa hizo zitaelekezwa katika hazina ya kuwatumia watu hawa fedha za matumizi kila mwezi.
Msaada mwingine wa kiasi cha Sh2.43 bilioni unawaendea wafanyabiashara wadogo kama ruzuku za kuwawezesha kuendelea na shughuli zao.
Na Sh600 milioni zitaelekezwa kwa sekta ya biashara ili kufanikisha kupatikana kwa chakula na dawa zinazohitajika kwa wenye mahitaji.
“Umoja wa Ulaya unasimama na Kenya wakati huu mgumu. Hii ni kwa sababu tunatambua athari za janga hili kwa maisha ya raia,” akasema Balozi wa EU nchini Simon Mordue.
Akaongeza: “Leo, kupitia misaada kama hii, tunalenga kubadilisha maisha ya jamii mbalimbali kote nchini Kenya na katika mitaa ya mabanda jijini Nairobi ambazo zimeathirika na janga hili. Aidha, misaada hii itasaidia kuimarisha uhusiano baina yetu na Kenya,” akaongeza.