Kimataifa

Furaha kwa Waisraeli na Wapalestina mkataba sasa ukianza kutekelezwa

Na MASHIRIKA January 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAMALLAH, WEST BANK

BAADA ya miezi 15 ya huzuni na wasiwasi, mateka watatu raia wa Israel waliokuwa wakizuiliwa na kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza walirejea nyumbani huku Wapalestina 90 waliokuwa wakizuiliwa katika magereza ya Israel pia wakiachiliwa huru.

Hii ni baada ya mkataba wa kusitishwa kwa vita kati ya Israel na Hamas kuanza kutekelezwa Jumapili.

Kwa mara ya kwanza, anga za Ukanda wa Gaza na Israel zilikuwa tulivu na Wapalestina walianza kurejea katika mabaki ya nyumba zao walikotoroka baada ya vita kuanza mnamo Oktoba 7, 2023.

Wapalestina hao waliungana na jamaa zao waliowaacha nyuma na wakakaribishwa kwa furaha kubwa.

Isitoshe, kwa mara ya kwanza vikwazo vilivyowekwa na Israel viliondolewa na malori 600 yaliyobeba chakula cha msaada, na mahitaji mengine, yaliingia katika Ukanda wa Gaza ulioharibiwa na vita.

Mkataba wa kukomesha vita ulioanza kutekelezwa Jumapili ulirejesha matumaini ya kukoma kabisa kwa vita kati ya Israel na Hamas.

Lakini nchini Israel, furaha ya kuachiliwa kwa mateka Emily Damari, Romi Gonen na Doron Steinbrecher na kuungana na familia zao ilikatizwa na maswali kuhusu hatima ya Waisraeli wengine 100 waliotekwa mnamo Oktoba 7, 2023 na wangali wanazuiliwa Gaza.

Ni siku ambayo wapiganaji wa Hamas walifanya mashambulio kadhaa kusini mwa Israel.

Baadhi ya Wapalestina waliokuwa wakizuiliwa katika magereza ya Israel waliposhindwa kudhibiti furaha yao wakiwa ndani ya basi baada ya kuachiliwa huru kufuatia kusitishwa kwa mapigano ya muda mrefu kati ya Israel na kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza. Picha|Reuters

Damari, Gonen na Steinbrecher wanatarajiwa kusalia hospitalini kwa siku kadhaa wakipokea matibabu.

Watatu hao ni miongoni mwa Waisraeli 33 mateka wanaotarajiwa kuachiliwa huru ndani ya wiki sita zijazo kulingana na mkataba huo.

Mateka wote walioachiliwa huru sasa wanatarajiwa kuendelea na shughuli zao za kawaida baada ya wao kupata afueni.

Mkataba huo pia unajumuisha kusitishwa kwa vita na kuachiliwa huru kwa Wapalestina 2,000 na kuwasilishwa kwa mafuta na misaada mingine Gaza.

Hata hivyo, kitachofanyika baada ya awamu ya kwanza ya siku 42 ya mkataba huo hakijulikani.

Awamu zijazo za utekelezaji wa mkataba huo zinajumuisha kuachiliwa huru kwa mateka, wafungwa na kusitishwa kabisa kwa vita.

Lakini Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema amepata hakikisho kutoka kwa Rais wa sasa wa Amerika, Donald Trump, kuwa Israel itaendelea kulishambulia kundi la Hamas “ikiwezekana”.

Hii ni licha ya kwamba ni Bw Trump na Rais aliyeondoka Joe Biden ndio walioiwekea Israel presha ikubali mkataba huo wa kusitishwa kwa vita.

Mnamo Jumapili, Waisraeli wengine walitazama runinga kuona jinsi wanawake walivyokuwa wakiachiliwa huru.

Picha hizo za runingani ziliwaonyesha maelfu ya Wapalestina, wakiwemo wapiganaji wa Hamas, wakivalia vitambaa vya kijani vichwani.

Wapiganaji hao walikuwa wakiwapokeza mateka hao kwa Shirika la Msalaba Mwekundu katika barabara moja jijini Gaza City.

“Taifa lote la Israel linawapokea,” Netanyahu aliwaambia mateka hao walioachiliwa huru.

Naye Waziri wa Usalama wa Kitaifa, Itamar Ben-Gvir, aliyejiuzulu Jumapili kutoka serikali ya Netanyahu, alisema taifa la Israel “linafurahi” kufuatia kuachiliwa huru kwa mateka hao.

Katika video iliyotolewa na serikali ya Israel, wanawake walionekana wakitoa machozi ya furahi wakiwakumbatia watu wa familia zao.