Kimataifa

G20: Ramaphosa apuuzilia mbali tishio la Rais Trump

Na MASHIRIKA December 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

JOHANNESBURGE, Afrika Kusini

RAIS wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amepuuzilia mbali tishio la Rais wa Amerika Donald Trump la kuizima nchi yake kuhudhuria Mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa Nchi 20 Kuu Duniani (G20) mwaka ujao, 2026.

Trump alisusia mkutano wa G20 uliofanyika kati ya Novemba 22 na 23 jijini Johannesburg.

Rais huyo wa Amerika akisema alikosa kufika katika mkutano huo kutokana na madai kuwa serikali ya Afrika Kusini, inayoongozwa na Weusi, imekuwa ikidhulumu Wazungu, walio wachache.

Mnamo Jumatano wiki jana, Trump alisema kuwa Afrika Kusini haitaalikwa katika mkutano wa G20 ukaofanyika Florida, Amerika, mwaka ujao.

Hii ni kwa sababu, Afrika Kusini ilidinda kukabidhi urais wa kundi la G20 kwa afisa wa cheo cha juu katika ubolozi wa Amerika nchini humo aliyehudhuria kikao cha kufungwa kwa mkutano wa mwezi jana.

Lakini Afrika Kusini ilikana madai hayo ikieleza alipitisha urais wa kundi hilo kwa afisa mmoja katika ubalozi wa Amerika jijini Johnnesburg.

“Afrika Kusini itasalia kuwa mwanachama kamili wa G20 na itahudhuria mkutano ujao jimboni Florida, Amerika,” Ramaphosa akasema kwenye hotuba kwa taifa Jumapili.

Aidha, alipuuzilia mbali madai kuwa serikali yake inawadhulumu rais Weupe nchini humo.