Gari la Papa Francis kugeuzwa kliniki tamba na kupelekwa Gaza kusaidia watoto
VATICAN CITY, Vatican
VATICAN inakamilisha mipango ya kulisafirisha gari maalum alilolitumia Hayati Papa Francis hadi Ukanda wa Gaza kutumika kama kliniki tamba ya kutoa matibabu kwa watoto wanaoathirika na vita vinavyoendelea eneo hilo.
Hatua hiyo inaafiki wosia wa kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki, kabla ya kifo chake.
Kabla ya kupelekwa Gaza, gari hilo, maarufu kama “popemobile” litaundwa upya na kuwekwa vifaa mbalimbali vya matibabu.
Gari hilo maalum lilitumika na Papa Francis kuwafikia na kuwabariki watu sehemu mbalimbali ulimwenguni alikozuru.
Aidha, ni gari hilo lilisafirisha maiti yake hadi mahala alikozikwa katika Kanisa la Basilica of St Mary Major, jijini Roma, nje ya Vatican mnamo Aprili 26.
“Ilikuwa ni matamanio yake ya mwisho, kwa watu ambao hakukoma kuwaombea, kwamba gari hilo litumike kuwahudumia,” shirika la habari Vatican News likasema Jumapili.
Karibu watoto milioni moja wanakabiliwa na njaa pamoja na magonjwa katika Ukanda wa Gaza baada ya kuporomoka kwa mfumo wa utoaji huduma za afya.
Hii ni kutokana na vita mapigano yanayoendelea katika ukanda huo kati ya Israel na kundi la Hamas.
“Watoto sio takwimu. Wao ni binadamu na kila moja wao anafaa kulindwa,” Papa Francis aliwahi kusema.
IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA