Gen Z 10 wajitosa uwanjani Uganda kupigania urais na mkongwe Museveni
VIJANA 10 wa kizazi cha sasa, almaaruf Gen Zs, ni miongoni mwa zaidi ya watu 50 waliojitokeza kutaka kushindana na Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi wa urais Januari mwaka ujao.
Mwaniaji mchanga zaidi ni Jorine Najjemba mwenye umri wa miaka 20, aliyekamilisha kidato cha sita mwaka jana.
Mwanadada huyo ni miongoni mwa wawaniaji waliochukua stakabadhi za uteuzi wa urais Jumatatu katika makao makuu ya Tume ya Uchaguzi (EC) katika eneo la Lweza viungani mwa Kampala.
Najjemba, anayewania kwa kauli mbiu ya; “Open Door New Uganda for Everyone” (Fungua Milango ya Uganda kwa Kila Mtu) alisema nchi hiyo imechoshwa na uongozi wa sasa na yu tayari kutoa uongozi mbadala.
“Tumechoshwa na uongozi wa watu wadhalimu na hasira, tunataka uongozi wa watu wanaoelewa mahitaji ya raia, watu wanaoongozwa na utu na ubinadamu. Na yule anaweza kuleta uongozi huo si mwingine ila ni mimi. Naomba raia waniunge mkono licha ya kwamba mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 20 pekee,” akawaambia wanahabari.
Rais Museveni, mwenye umri wa miaka 81 ameongoza Uganda kwa karibu miongo minne, tangu 1986.
Anatarajiwa kuwania tena katika uchaguzi huo wa 2026 kusaka nafasi ya kuongoza kwa muhula wa saba.
Gen Zs wengine ambao walichukua fomu za uteuzi kutoka kwa tume ya EC ni pamoja na Bi Abigail Ayeza, 22, Pauline Nankambwe, 24, ambaye ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Kikristo Uganda (UCU) na Wycliffe Kasaijja, 24.
Wengine ni; Alvin Mivue (mwanafunzi anayesomea uanasheria) na David William Magezi, 25, ambaye ni Menaja wa Idara ya Huduma za Wafanyakazi (HR).
Katiba ya Uganda ilifanyiwa marekebisho mnamo 2017, hatua iliyoondoa hitaji kuhusu umri wa juu zaidi kwa mtu kuwania urais.
Kabla ya marekebisho hayo, kipengele cha 102 (b) cha Katiba ya 1995 ya Uganda kilisema kuwa mtu hatahitimu kuwania ikiwa hajatimu umri wa miaka 35 au ikiwa umri wake unazidi miaka 75.
Aidha, umri wa chini zaidi kwa mtu kuhitimu kuwania urais ulipunguzwa kutoka miaka 35 hadi 18, awe amehitimu kimasomo hadi kiwango cha “A” levels na aungwe mkono na angalau wapiga kura 100 kutoka thuluthi mbili za wilaya zote nchini Uganda.
Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa nchini Uganda wanasema kuwa hatua ya vijana wengi kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha urais inaashiria kuwa wamekosa imani kwa uongozi wa sasa.
“Hii inamaanisha kuwa vijana wanataka mabadiliko, wanataka uongozi unaojali masilahi yao kwani wao ndio wengi. Wamechoshwa na uongozi wa kizazi cha watu wazee,” anasema Sarah Birete, ambaye ni mkuu wa shirika la Centre for Constitutional Governance.
Naye Mkenya Martin Andati anabashiri kuwa kujitokeza kwa idadi kubwa ya vijana wa Gen Zs wenye nia ya kuwania urais Uganda kutawachochea wenzao nchini Kenya kuiga mfano huo 2027.
“Tuliona vijana kutoka taifa hilo la Uganda, na mataifa mengine Afrika, wakiiga maandamano ya Gen Zs wa Kenya Juni mwaka jana. Vivyo hivyo, huenda wimbi la sasa likafika Kenya 2027,” anasema mchanganuzi huyo wa masuala ya siasa na uongozi.
Hata hivyo, Bw Andati ameelezea hofu kwamba Rais Museveni, kama kawaida yake, atatumia nguvu za dola kuzima ndoto za vijana hao.
“Hapa Kenya Rais William Ruto pia atatumia mbinu kadhaa ikiweno “kuwanunua” vijana watakaodiriki kutangaza nia ya kumpinga. Vile vile, huenda akatumia mbinu ya kuwadhamini baadhi ya wagombeaji ili kama njia ya kudhoofisha upinzani dhidi yake,” anaongeza Bw Andati.