Kimataifa

Gen Z wa Madagascar watofautiana na jeshi baada ya kung’oa rais

Na REUTERS October 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MGAWANYIKO umeanza kati ya Gen Z na uongozi mpya wa jeshi Madagascar kutokana na mwelekeo ambao taifa hilo linastahili kuchukua baada ya kufurushwa kwa Rais Andry Rajeolina.

Kanali Michael Randrianirina ambaye alikuwa mkuu wa jeshi, aliapishwa kama rais Ijumaa iliyopita, siku tatu baada kurejesha udhabiti nchini humo kutokana na wimbi la maandamano.

Michael anastahili kuongoza kwa miaka miwili kisha kuweka mifumo bora ya kuandaliwa kwa uchaguzi ambao ni wenye huru na haki.

Hata hivyo, baadhi ya Gen Z ambao waliandaa maandamano ya kumng’oa Rajeolina, hawajaridhishwa na uongozi wa jeshi.

“Malengo yao sasa yametoka katika kuwalinda raia na kutwaa mamlaka. Sisemi nawapinga lakini mwelekeo huu hauturidhishi,” akasema Kiongozi wa Gen Z aliyeongoza maasi Olivia Rafetison.

Pamoja na wengine wameingiwa na wasiwasi iwapo matakwa yao yatashughulikiwa ama jeshi litaongoza tu kama Rajeolina.

Usiku wa mapinduzi, Michael alikutana na Rafetison na viongozi wengine wa Gen Z.

“Wakati huo alisema wanatusikiza,” akasema Rafetison kabla ya kufichua kuwa kwa sababu siku hiyo wanajeshi walikuwa wamechoka waliahirisha mkutano wa kuzungumzia matakwa yao.

“Natumai watafuatilia kwa sababu huu si mwisho wa mapambano. Tunapigania sana mabadiliko ya nchi wala si kubadilisha rais moja hadi kwa mwengine bila hatua zozote kupigwa,” akaongeza kiongozi huyo wa Gen Z.

Kundi moja la Gen Z kwenye Facebook lenye wanachama zaidi ya 18,000 nalo limeonya jeshi kuwa hawataki uongozi wao.

“Hao wanajeshi hawatilii manani maslahi ya raia bali yao wenyewe. Bado hatujamaliza mapambano hadi tuhakikishe kuwa kila kitu kiko sawa,” akasema Mkuu wa kundi hilo Tonga Saina.