Gen Z wa Uganda waliokamatwa washtakiwa ‘kukera’ serikali
KAMPALA, UGANDA
WATU kadhaa wakiwemo vijana wa GenZ waliojitokeza jana kuandamana baada ya serikali ya Uganda kupiga marufuku maandamano nchini humo wamefunguliwa mashtaka.
Watu hao 60, akiwemo mtangazaji maarufu wa radio na televeshini walifikishwa mahakamani chini ya ulinzi wa polisi kwa mashtaka yakiwemo yale “ya kuwa kero” kwa serikali.
Hapo jana, vikosi vya usalama nchini humo viliwazuia vijana kadhaa jijini Kampala waliokuwa wakishiriki katika maandamano hayo.
Waandamanaji hao walisema walijitokeza katika barabara za jiji hilo kupinga jambo walilolitaja kama mwenendo wa watawala wa nchi hiyo kutopambana na ufisadi na ukiukaji wa haki za binadamu.
Video moja iliyopakiwa katika akaunti ya X ya NTV Uganda ilionyesha kundi la vijana likikabiliwa na kunaswa na polisi walipokuwa wakiandamana.
Waandamanaji hao walibeba mabango na kutoa kauli za kupinga ufisadi. Mmoja alivalia tishati yenye maneno “Speaker Must Resign” (Sharti Spika Ajiuzulu).
Picha zilizopeperushwa na NTV Uganda zilionyesha magari ya wanajeshi yenye vifaa vya kukinga risasi yakizunguka maeneo ya karibu na bunge.
Rais Yoweri Museveni, ambaye ameliongoza nchi hiyo kimabavu kwa takriban miongo minne, alikuwa ameonya mwishoni mwa Juma kwamba waandamanaji “wanacheza na moto”.
Serikali ya Uganda, kupitia Idara ya Polisi, ilipiga marufuku maandamano hayo, ikidai kuwa na habari za kijasusi kwamba vijana wahalifu walikuwa wanapanga kuingilia maandamano ili kupora na kuharibu mali ya umma na mali ya kibinafsi.
Maafisa wa Jeshi la Uganda na polisi walipelekwa kushika doria karibu na majengo ya bunge na maeneo kadhaa katikati mwa jiji la Kampala kwa lengo la kuwazuia waandamanaji hao.
Msemaji wa polisi Kituuma Rusoke alisema mamlaka hazitoruhusu maandamano yoyote ambayo yanatishia “amani na usalama wa Uganda”.
Mnamo Jumatatu, polisi walizingira afisi za chama kikuu cha upinzani nchini Uganda.
Serikali ilidai kuwa chama hicho ndicho kilihusika katika maandalizi ya maandamano hayo ya kupinga serikali. Baadhi ya maafisa wa chama hicho walizuiliwa, wakiwemo wabunge wake.
Chama hicho, National Unity Platform (NUP) kilikana madai hayo kikiyataja kama ambayo “hayana msingi wowote”.
Kiongozi wa chama hicho Robert Kyagulanyi (maarufu kama Bobi Wine) alisema baadhi ya maafisa wake walidhulumiwa na maafisa hao wa usalama walipokuwa wakikamatwa.
“Waoga hawa wamegeuza makao makuu ya National Unity Platform kuwa kambi ya jeshi,” Bobi Wine akaandika katika mtandao wa X.
Hongo ni tatizo kubwa nchini Uganda, huku kukiwa na kashfa kadhaa zinazohusisha viongozi wa ngazi ya juu na maafisa wa umma, na nchi hiyo iliorodheshwa nafasi ya 141 kati ya nchi 180 kwenye ripoti ya shirika la Transparency International linalokabiliana na ufisadi.