Kimataifa

Gen Z wazua ghasia Madagascar wakitaka Rais Andry Rajoelina ang’atuke mamlakani

Na REUTERS, CHARLES WASONGA September 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ANTANANARIVO, Madagascar

POLISI nchini Madagascar Jumatatu, Septemba 29, 2025 waliwakabili kwa vitoza machozi maelfu ya waandamanaji waliorejea barabarani kushiriki awamu ya tatu ya maandamano kupinga kukatwa kwa huduma za maji na umeme.

Wengi wa waandamanaji hao, idadi kubwa wakiwa vijana wa kizazi cha kisasa, maarufu kama Gen Z, walishinikiza kujiuzulu kwa serikali ya nchi hiyo.

Huku wakionekana kuiga maandamano ya Gen Z katika mataifa ya Kenya na Nepal, waandamanaji walijitokeza kwa wingi zaidi, hali ambayo haijawahi kushuhudiwa katika Kisiwa hicho kilichoko Bahari ya Hindi.

Wadadisi wanasema tukio hilo ni changamoto hatari zaidi kumkabili Rais Andry Rajoelina tangu alipochaguliwa tena 2023.

Kufuatia fujo hizo, watawala walitangaza amri ya kutotoka nyakati za usiku kuanza Alhamisi maandamano jijini Antananarivo yalipokumbwa na fujo kubwa.