Hafla ya kuapishwa kwa Rais yasusiwa baada ya maandamano ya miezi kadhaa
MSUMBIJI, AFRIKA KUSINI
RAIS wa Msumbiji Daniel Chapo ameahidi kupunguza idadi ya wizara huku akiahidi kushughulikia ajira kwa vijana pamoja na kuimarisha sekta za afya na elimu.
Akizungumza wakati wa kuapishwa kwake, Rais Chapo alisema kuwa wakati wa siasa umepita na akawaomba raia wa nchi hiyo wampe nafasi ya kutekeleza ajenda ya serikali yake.
“Ninaomba tukumbatie mazungumzo kukabili changamoto ambazo zinatusibu. Ni kupitia kuongea ndipo tutakuwa na taifa ambalo lina umoja kisha tupige hatua kimaendeleo,” akasema Rais Chapo.
Kiongozi huyo alilishwa kiapo cha urais kwenye hafla ambayo ilihudhuriwa na wananchi wachache (1,500) baada ya maandamano kushuhudiwa nchini humo kwa miezi kadhaa.
Alishinda urais kwenye uchaguzi ulioandaliwa mnamo Oktoba 9 kupitia chama cha Frelimo ambacho kimeongoza nchi hiyo tangu ijinyakulie uhuru mnamo 1975.
Upinzani umekuwa ukidai ndio ulishinda uchaguzi huo ambao waangalizi nao wamesema haukuwa huru na haki na ulijaa udanganyifu na wizi wa kura.
Ingawa hivyo, Frelimo ilikanusha kuwa imeshiriki wizi wa kura huku ikishutumu upinzani kwa kulenga kusambaratisha nchi hiyo kwa kutumia tofauti za kisiasa.
Maafisa wa usalama walimwagwa Maputo katika hafla ya kuapishwa kwa Rais.
Chapo ili kutibua jaribio lolote la maandamano ambayo yalikuwa yamepangwa na upinzani.
Ilikuwa hafla ambayo idadi ya wananchi ilikuwa chini mno ikilinganishwa na sherehe nyingine za hapo nyuma ambapo marais walikuwa wakiapishwa.
Marais kutoka Afrika nao walionekana kususia hafla hiyo huku Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini na Umaro Sissoco Embalo wa Guinea wakiwa Marais pekee waliohudhuria.
Kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane ambaye aliibuka wa pili kwenye kura hiyo naye ametoa wito kwa wafuasi wake waendelee na maandamano.